Timu ya Azam FC imeanza vyema michuano ya kuwania kombe la Mapinduzi baada ya kuifunga 3-1 timu ya Kikwajuni katika mchezo wa kwanza wa michuano hiyo uliochezwa kwenye uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar.

Tunaomba radhi kwa taarifa hii kuchelewa kutokana na matatizo ya internet network, unapoisoma jenga picha kama leo ni jumatatu siku Azam ilipocheza na Kikwajuni

Azam FC ni moja ya timu zinazoshiriki michuano hiyo inayoumuisha timu tatu kutoka Tanzania bara na timu tano kutoka visiwani Zanzibar kwa akiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Mapinduzi yanayoadhimishwa Januari 12 kila mwaka.

Katika mchezo wa leo Azam FC walianza kushambulia lango la Kikwajuni dakika ya nane ya mchezo kwa shuti lililopigwa na John Bocco lakini halikuweza kuingia wavuni, dakika ya 12 Kipre Tchetche akiunga krosi ya Salum Aboubakari na kutumia uzembe wa mabeki wa Kikwajuni aliifungia Azam goli la kwanza katika mchezo huo.

Goli hilo ambalo ni la kwanza kwa muchuano ya mwaka huu, Kikwajuni hawakuwa nyuma wakitaka kusawazisha dakika ya 27 Ramadhani Hussein alipiga shuti langoni mwa Azam lililotoka nje.

Azam wakionyesha kiwango cha juu katika mchezo huo walipata goli la pili dakika ya 31 ikiwa ni kazi nzuri iliyotengenezwa na Tchetche na kumkuta John Bocco aliyefunga goli hilo lililoamsha nguvu zaidi kwa Azam yenye lengo la kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.

Kipindi cha pili timu zote zilibadilika na kucheza kwa nguvu zaidi Azam walifanya mabadiliko walitoka Abdulhalim Humud ambaye kipindi cha kwanza alifanya vizuri upande wa viungo nafasi yake ikachukuliwa na chipukizi Himid Mao, dakika ya 57 aliingia Samir Haji kuchukua nafasi ya John Bocco na dk 67 alitoka Michael Kipre akaingia Abdulghan Gulam.

Mabadiliko hayo yalipelekea Azam FC kupata goli la tatu kupitia kwa Khamis Mcha Vuali aliyewaacha mabeki na kipa wa Kikwajuni Rashid Haji na kuachia shuti lililotinga moja kwa moja wavuni.

Goli pekee la Kikwajuni lilifungwa na Haji Mwinyi  dk 81 kwa mpira wa adhabu baada ya beki wa Azam Waziri Salum kumwangusha Ahmed Maliki, goli hilo lilimaliza mchezo kwa Azam FC kuwa na pointi tatu katika kundi B lenye timu za Kikwajuni, Yanga na Mafunzo.

Baada ya mchezo wa leo Azam FC itacheza mchezo wake wa pili siku ya Jumatano dhidi ya Yanga ya Dar es Salaam kwenye uwanja huo, Kocha wa Azam FC Stewart Hall amesema matokeo ya mchezo wa leo yamewaweka vizuri katika kundi lao na kuanza maandalizi ya kucheza na Yanga kwenye mchezo ujao.

“Wachezaji wameonekana kuuzoea uwanja huu ambao hauko vizuri sana, naamini kwa mechi ya leo watafanya vizuri pia kwenye mchezo ujao tutakao kutana na Yanga, tunaamini tutashinda” alisema kocha huyo.

Kikosi Azam FC, Mwadini Ally, Agrey Moris, Erasto Nyoni, Ibrahim Shikanda, Waziri Salum, Humud/Mao, Michael Kipre/Gulam, Sure Boy, Mcha, Kipre, Bocco/Haji.