Timu ya Azam FC imetoka sare ya 1-1 na Mafunzo ya Zanzibar katika mchezo wa pili wa michuano ya kombe la Mapinduzi inayofanyika uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar.

Azam FC imefikisha pointi nne na kuongoza kundi B sawa na Mafunzo  wakitofautiana idadi ya magoli ya kufunga, ikifuatiwa na Yanga na Kikwajuni ambazo zilipoteza michezo yao ya kwanza.

Matokeo ya mchezo wa leo yameiweka vizuri Azam FC kuweza kuingia hatua ya nusu fainali ya michuano, katika mchezo huo kocha wa Azam FC alibadili kikosi tofauti na kile kilichoanza mechi ya kwanza.

Katika mchezo wa leo wachezaji wasiocheza mechi ya kwanza Gaudence Mwaikimba, Abdi Kassim ‘Babi’, Mrisho Ngassa, na Zahor Pazi walianza kipindi cha kwanza.

Wachezaji hao walicheza katika kiwango cha juu muda wote wa mchezo, Mafunzo walikuwa wa kwanza kupata goli dakika ya 12 lililofungwa na Jaku Joma akiunga mpira w akona iliyopigwa na Haji Hassan.

Mshambuliaji mahiri wa Azam FC, Mwaikimba aliisawazishia timu yake dakika ya 27 akiachia shuti lililomshinda kipa wa Mafunzo Selemani Janabi, Mwaikimba alitumia nafasi hiyo vizuri akiwa yeye na kipa na kuipatia goli timu yake.

Kipindi cha pili Azam FC walifanya mabadiliko walitoka Mrisho Ngassa, Abdi Kassim na Zahor Pazi nafasi zao kuchukuliwa na Michael Kipre, John Bocco na Khamis Mcha mabadiliko hayo yaliongeza kasi ya mchezo, dakika 78 Mwaikimba alipiga shuti likagonga mwamba na kutoka nje, hadi kumalizika kwa mchezo timu zote zilitoka sare ya 1-1.

Mwamuzi wa mchezo huo aliamuru kocha wa Azam FC atoke katika benchi la timu hiyo na kukaa jukwaani kutokana na kukiuka sheria za matumizi ya eneo la benchi la ufundi.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo kocha wa Azam, Stewart Hall alisema matokeo ya leo ni sehemu ya mchezo pia hayajawaharibia lengo lao la kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.

Amesema katika mchezo wa leo amebadilisha kikosi kuwapa nafasi wachezaji wote na kutumia nafasi hiyo kumjaribu Ngassa aliyekuwa majeruhi.

“Kiwango kilikuwa kizuri Ngassa ameanza vizuri mazoezi na ataendelea kucheza kwa muda mfupi hadi atakaporudi katika hali yake ya kawaida” aliongeza Stewart.

Azam watacheza mchezo wao wa kumaliza hatua ya makundi dhidi ya Yanga, mchezo unaotarajiwa kuwa mgumu kwa pande zote.

 

Azam FC: Mwadini Ally, Waziri Salum, Erasto Noni, Said Morad, Agrey Moris, Abdulhalim Humud, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’, Zahor Pazi/Khamis Mcha Mwaikimba, Abdi Kassim/John Bocco na Mrisho Ngassa/Michael Kipre