Maandalizi ya mapema kwa klabu ya Azam FC ndio chanzo cha kuanza vyema michuano inayoendelea ya kuwania kombe la Mapinduzi inayofanyika visiwani Zanzibar.

Gaudence Mwaikimba pichani atakuwa akiongoza safu ya ushambuliaji leo jioni akishirikiana na Zahoro Pazi na Mrisho Ngasa

Azam FC masaa machache yajayo itacheza mchezo wake wa pili dhidi ya timu ya Mafunzo na sio Yanga, mchezo kati ya Azam na Yanga umesogezwa mbele na kufanyika siku ya Ijumaa kutokana na sababu za waandaji.

Kocha wa Azam FC, Stewart Hall alisema wachezaji wake wameshaanza kuuzoea uwanja huo hivyo mechi zijazo wataendelea kufanya vizuri.

“Tumefanya mazoezi ya kutosha, timu ipo vizuri lakini uwanja ulikuwa tatizo, kwa sasa wachezaji wameshaanza kuuzoea uwanja huo” alisema Stewart.

Aliongeza kuwa kutokana na kutumia uwanja mbovu wameendelea kufanya mazoezi katika viwanja vinanyofanana na huo ili kujiweka imara zaidi na kuweza kukabiliana na timu yoyote.

Akizungumzia michuano hiyo, kocha Stewart alisema timu zote zinaonekana kujiandaa hivyo kupitia mechi hizo timu yake itakuwa katika kiwango kizuri.

Azam FC itashuka uwanjani ikiwa inaongoza kundi A kwa kuwa na pointi tatu sawa na timu ya Mafunzo ambayo iliifunga Yanga ya Dar es Salaam 1-0, Yanga io nafasi ya tatu huku Kikwajuni wakishika nafasi ya mwisho.

Mchezo mwingine wa kundi hilo utachezwa leo usiku kati ya Yanga itakayocheza na Kikwajuni.

Azam FC itakayoshuka dimbani leo ni Mwadini Ally, Erasto Nyoni, Waziri Salum, Aggrey Morris, Said Moradi, Humud Abdulhalim, Salum Abubakar, Mrisho Ngasa, Abdi Kassim, Gaudence Mwaikimba na Zahoro Pazi