Awali ya yote webmaster angependa kuwashukuru sana mashabiki wa kweli wa Azam FC kwa kuwa bega kwa bega na sisi katika kipindi chote cha misimu mitatu ya ushiriki wetu ligi kuu ya Tanzania. Hakika klabu yetu imekua sana kimuundo, miundombinu, vitendea kazi na nguvu kazi. Yote haya yasingepatikana bila nyinyi kwani mara zote ushauri wenu na uwepo wenu vimekuwa vikiwatia nguvu wakurugenzi na kujiona wana deni kwenu. AHSANTENI SANA.

Pichani juu ni Kipre Bolou Michale Wilfred, Nyota kutoka Ivory Coast na mmoja wa wachezaji tegemeo wa Azam FC akifunga goli la kwanza la Azam FC dhidi ya JKT Ruvu mbele ya Kiungo Mkabaji Mkongwe David Minja wa JKT Ruvu hii ilikuwa ni katika mechi ya kirafiki iliyochezwa Chamazi tarehe 30/12/2011. Azam FC ilishinda 3-0

Azam FC hivi sasa ina wachezaji 24 wa kikosi cha kwanza na wengine saba wakiwa nje kwa mkopo. Hivyo basi Azam FC ina wachezaji 31. Pia tuna timu za Vijana ambao wamegawika kama ifuatavyo wawili wana miaka 19, watano wana miaka 18, kumi wana miaka 17  na tisa wana miaka 16, pia kikosi kina wachezaji ishirini na sita wa chini ya miaka 14 hawa ni wakazi wa maeneo ya Mbande.

Huku tukianza mwaka 2012, Azam FC tunajivunia ukweli kwamba timu za Taifa za Under 17 U-20 na U-23 wakati wote zimekuwa zikiundwa na wachezaji wengi toka Azam FC, na safari hii ndiyo tumetia for kwa kuwa na vijana tisa ambao ni wachezaji wa kikosi cha Taifa cha Under 17.  Huu ni mchango mkubwa sana kwa taifa letu na kama klabu tunadhani tumetimiza wajibu wetu.

Azam FC kwa mwaka 2011 imekuwa klabu iliyoongoza kwa kutoa wachezaji wengi timu ya Taifa ya Tanzania. Wachezaji hawa ni Mwadini Ally, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Jabir Aziz, Mrisho Ngasa, Ramadhani Chombo na John Bocco. Tunatarajia idadi hii itaongezeka mwaka 2012 na kwetu ni ufahari kushiriki majukumu ya kimataifa.

Katika mashindano ya CECAFA Challenge msimu huu, Azam FC ilitia fora kwa kutoa wachezaji wengi zaidi kwenye mashindano hayo. Rekodi hii pia tuliishikilia msimu wa 2009 kule Nairobi ambako tulikwa na wachezaji saba. Msimu uliopita Dar es Salaaam ambapo tulikuwa na wachezaji 10 na msimu huu tumeongeza wachezaji wawili na kuwa na wachezaji 12 ambao ni Mwadini Ally,  Erasto Nyoni, Waziri Salum, Aggrey Morris, Said Moradi, Abdulghani Ghulam, Abdulhalim HUmud, Ibrahim Mwaipopo, Ramadhani Chombo, Mrisho Ngasa, Khamis Mcha na Selemani Kassim.

Azam FC ni timu inayoamini kuwa Soka halijengwi kwa kinachoitwa FITNA ZA SOKA au Rushwa michezoni. Azam FC itaendelea kuboresha kikosi chake, kuboresha benchi la ufundi na kuboresha timu ya watendani pamoja na miundombinu kama  Gym, Kambi, Uwanja nk lakini haitathubutu kujiingiza kwenye propaganda za FOOTBALL FITNA na msimamo wa Bodi ya wakurugenzi wa Azam FC kama wanavyofahamika na watanzania wengi ni kuwa Be the BEST and you will ACHIEVE the BEST.

Azam FC pia inaamini kuwa mafanikio ya kweli kwenye soka hayajengwi kwa siku moja bali kwa kipindi kirefu kama yale ya Manchester United Chini ya Feguson au Barcelona

Kumekuwa na maswali mengi sana kuhusu kwa nini Azam FC haitumii wachezaji wake vijana? lakini wanaohoji maswali hayo wanapaswa kuelewa kuwa Azam FC ina umri wa miaka mitatu tuu tangia tuingie ligi kuu na tuamue kufanya biashara ya soka kwa umakini. Miaka hiyo mitatu kwa kijana anayezungumzwa hapa kama aliibuliwa na Azam FC akiwa na miaka 14 hivi sasa atakuwa na miaka 17 umri ambao bado anahitaji kujifunza. Hata hivyo tunapenda kuwafahamisha mashabiki wetu kuwa msimu huu tumevunja rekodi nyingine kwa vijana wetu takribani watano wa Under 17 kuazimwa na timu za ligi kuu. Haya ni mafanikio kwetu na kwao na tunaamini msimu utakapoisha watakuja wakiwa wamejifunza kitu flani.

Tunasema ni mafanikio kwani vijana tunaowaona Barcelona/Manchester united au Arsenal hupitia kuazimwa kwanza na timu nyingine ndogo ili kupata fursa ya kucheza na kupata uzoefu kisha hurudi klabuni wakiwa kamili. Vijana wa Azam FC walio nje kwa mkopo ni Omari Mtaki – JKT Oljoro, Simon Msuva, Jamal Mnyate na Tumba Swedi – Moro United, Mau Bofu Ally – Kagera Sugar, Sino Augustino – African Lyon na Daudi Mwaisongwe, Ibrahim Rajab Jeba na Ismail Adam Gambo Villa Squad. Kati ya hao waliotajwa hapo juu Ismail Adam Gambo, Simon Msuva na Ibrahim Rajab Jeba ni chipukizi walioshiriki Uhai Cup na sisi Msiku huu na kufika fainali.

Azam FC inajivunia kuwa na Golikipa Aishi Salum mwenye miaka 17 ambaye amepandishwa kikosi cha kwanza, beki Haji Samih Nuhu ambaye ni zao halisi ya Academy yetu kama ilivyo kwa Himid Mao. Pia tunajivunia wachezaji kama John Bocco, Jamal Mnyate ambaye tumemtoa kwa mkopo Moro United na Salum Abubakar, Luckson Kakolaki na malika Ndeule ambaye tumempeleka mkopo Villa Squad kwa kuwa ni vijana wadogo ambao historia yao ya soka imeanzia Azam FC na Azam FC ingependa kuwatengeneza, kuwaenzi na kudumu nao muda mrefu zaidi kutokana na nidhamu yao, vipaji vyao na uelewa wao.

Azam FC inajivunia mafanikio makubwa ya kikosi chetu cha vijana ambapo katika mashindano ya Uhai Cup ambayo yamefanyika mara nne, tumeingia fainali mara tatu, Azam FC imetwaa kombe mara mbili na mara moja imeshika nafasi ya pili. Haya ni mafanikio makubwa sana na hatuna budi kujipongeza.

Msimu wa mwaka 2012 tunawaahidi kukwea kwa timu yetu ngazi moja mbele toka hapa tulipo yaani nafasi ya tatu ambayo tumekuwa tukiishikiria kwa misimu miwili hadi Ubingwa au angalau nafasi ya pili. Lakini kwa kuanzia tungependa kutwaa kombe la Mapinduzi ambalo tunaenda kushiriki kuanzia kesho.

Azam FC- Timu Bora Bidhaa Bora toka Bakhresa Group of Companies

Azam FC – Tucheza Pamoja kwa Furaha