Timu ya Azam FC imeendeleza ubabe kwa Yanga baada ya kuifunga timu hiyo 2-0 katika mchezo wa kirafiki ulioandaliwa kwaajili ya kuchangisha fedha za kusaidia Chama cha Walemavu uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo wa kijamii umeandaliwa maalum kusaidia chama hicho kukusanya kiasi cha shilingi milioni 30 zitakazotumika kutolea vifaa vya walemavu vilivyokwama bandarini.

Katika mchezo huo uliovuta hisia za watu wengi mchezaji wa Azam FC, Mrisho Ngassa leo alikuwa kivutio kutokana na kandanda la hali ya juu akifunga goli safi na kutengeneza lingine lililofungwa na Gaudensi Mwaikimba kwa penati.

Azam walianza kuutawala mchezo mwanzoni kipindi cha kwanza ambapo dakika ya 11 na 26 Abdulhalim Humud na Abdi Kassim walikosa kufunga kupitia mpira wa adhabu waliyopiga nje.

Dakika ya 45 mshambuliaji Gaudence Mwaikimba aliyejiunga na Azam katika usajili wa dirisha dogo aliifungia timu hiyo goli la kwanza kwa mkwaju wa penati baada ya mabeki wawili wa Yanga kumwangusha Ngasa ndani ya eneo la penati.

Goli hili lilizipeleka timu zote mapumziko Azam wakiongoza 1-0, kipindi cha pili Azam FC walifanya mabadiliko walitoka Bolou Kipre, Abdulhalim Humud na Kipre Tchetche nafasi zao kuchukuliwa na Jabir Aziz, Salum Aboubakar 'Sure Boy' na Zahor Pazi.

Mabadiliko hayo yalibadili mchezo kwa Azam FC yaliboresha sehemu ya kiungo na kutengeneza nafasi nyingi ambayo dakika ya 57 zilizaa matunda na kupatikana goli la pili lililofungwa na Ngasa kufuatia mpira wa kona iliyopigwa na Abdi Kassim Babi.

Baada ya goli mpira ulibadilika na kuwa wa kasi kwa timu zote Yanga wakitafuta nafasi ya kusawazisha Azam wao walitafuta nafasi ya kuongeza goli jingine huku wakicheza kandanda safi.

Wachezaji wa Yanga, Omega Seme, Athman Idd 'Chuji' na Idrisa Rashidi walikosa magoli kwa kupiga mashuti nje n amengine kuokolewa na kipa wa Azam, Mwadin Ally.

Katika mchezo huo wachezaji waliojiunga dirisha dogo Abdi Kassim, Bolou Kipre na Gaudence Mwaikimba wameonyesha kiwango kizuri na kuwa na mahusiano mazuri na wachezaji wengine wa klabu hali iyopelekea kupatikana kwa matokeo hayo mazuri kwa Azam FC inayojiandaa na michunao ya Mapinduzi Cup na ligi kuu.

Azam FC walioshiriki katika mchezo huo wa kijamii Mwadini Ally, Aggrey Moris, Erasto Nyoni, Bolou Kipre/ Jabir Aziz , Said Morad, Waziri, Kipre Tchetche/Zahor Pazi, Abdulhalim Humud/Sure Boy, Gaudence Mwaikimba/Ibrahim Shikanda, Abdi Kassim 'Babi'/Samir Haji Nuhu na Mrisho Ngassa/Khamis Mcha