Timu ya Azam FC imeendelea na mazoezi ya kujiandaa na ligi kuu pamoja na michuano ya Kombe la Mapinduzi 2012 yanayotarajiwa kuanza mapema mwaka ujao.

Katika mazoezi hayo yanayofanyika kwenye uwanja wa Azam Chamazi, wachezaji wote wanaendelea na mazoezi isipokuwa wale waliokuwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania bara ‘Kilimanjaro Stars’ ambao wapo katika mapumziko watajiunga kwa mazoezi siku ya Ijumaa.

Akizungumza na www.azamfc.co.tz kocha wa Azam, Stewart Hall amesema wachezaji wanaendelea na mazoezi ya kila siku yanayojumisha mazoezi ya gym, misuli na uwanjani.

“tunafanya mazoezi  kujiandaa kwa michezo ijayo unajua tunakabiliwa na mechi za ligi kuu pamoja na kombe la Mapinduzi hivyo kwa maandalizi haya ya mapema yatasaidia kujenga timu imara” amesema Stewart.

Kocha ameongeza kuwa mbali na kufanya mazoezi hayo watakuwa na mechi za kirafiki za kujipima, ya kwanza itakuwa Jumamosi hii na mechi nyingine itachezwa tarehe 20 mwezi huu dhidi ya timu ya Yanga.

“Mchezo wa wiki hii bado tupo katika maongezi na vilabu vitatu vya ligi kuu, lakini mechi na Yanga hiyo itanyika Desemba 20” aliongeza kocha huyo.

Akizungumzia kiwango cha wachezaji Gaudence Mwaikimba, Bolou Kipre na Abdi Kassim ‘Babi’ waliojiunga na klabu hiyo, kocha alisema wapo katika kiwango kizuri na anaamini wataleta mabadiliko katika timu.