Timu ya Azam Academy imeibuka mshindi wa pili katika mashindano ya vijana chini ya miaka 20 'Uhai Cup' baada ya kufungwa penati 6-5 na Simba B kwenye mchezo wa fainali uliochezwa uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.

Hii ni mara ya kwanza kwa timu ya Simba B kutwaa ubingwa wa michuano hiyo iliyoanzishwa miaka minne iliyopita.

Katika mchezo huo uliokuwa wa ushindani na kukutanisha timu zenye viwango vizuri, walimaliza dakika 120 bila kufungana na mwamuzi wa mchezo huo Juma Seif kuamuru zipigwe penati ili kupatikana mshindi.

Timu zote zilimaliza penati zote tano kwa kufunga ndipo zikaanza penati za nyongeza ambayo mlinzi nyota wa Azam, Dizana Issa alikosa penati hiyo kwa kupiga mpira nje na kuwapa nafasi Simba iliyotumiwa vyema na mchezaji William Luciana aliyefunga penati ya sita na kumaliza mchezo huo.

Azam wakicheza kwa mara ya tatu fainali ya mashindano hayo, walitumia mchezo huo kuonyesha viwango vyao kwa kucheza kandanda safi vipindi vyote vya mchezo huo.

Golikipa wa Azam, Aishi Mfulula amekuwa golikipa bora wa mashindano haya wakati mshambuliaji Simon Msuva akipokea kiatu kwa kuwa mfungaji bora, wote walizadiwa kiasi cha sh 300,000 kila mmoja.

Bingwa Simba amekabidhiwa kombe na sh Milioni 1.5 na medali ya dhahabu, Azam wamepata sh milion 1na medali ya fedha wakati mshindi wa tatu Serengeti Boys (U17) wakiondoka na sh 500,000 na medali ya shaba, Mwamuzi bora wa mashindano hayo ni Juma Seif wakati mchezaji bora ametajwa Ramadhani Singano wa Simba na kukabidhiwa sh 400,000.

Kocha wa Azam, Vivek Nagul amesema kupata ushindi wa pili ni moja ya mafanikio kwa timu yake kwa kuwa inaundwa na wachezaji walio chini ya miaka 17 wakati timu zilizoshiriki zikiwa na wachezaji wengi wenye miaka chini ya 20.

“Japo tumekosa ushindi lakini ni faraja kwangu, fainali ilikuwa nzuri sana wachezaji wangu wamejitahidi nafasi zote lakini mwisho ilikuwa lazima mshindi apatikane” alisema Vivek.

Akieleza kukosa penati kwa mchezaji Dizana kocha alisema, ni bahati mbaya kwa mchezaji kukosa penati japo imetugharimu kukosa ubingw ahuo lakini nafasi tuliyofikia tuna kitu cha kujivunia.

Aliwataka wachezaji wake wasife moyo na kubweteka kwa kupata nafasi hiyo ila wajitahidi kuimarika zaidi ili waweze kufanya vizuri kwenye mashindano yajayo.

Azam walitwaa kombe hilo mara mbili 2008 na 2009 kabla ya mwaka 2010 kuchukuliwa na Ruvu Shooting, michuano hiyo mwaka huu imeshirikisha timu 15.

Kikosi Azam FC.Aishi Mfulula, Kelvin Idd, Braison Nkulula, Ibrahim Juma 'Jeba', Ally Kaijage, Mgaya Jafari, Dizana Issa, Mohamed Hussein, Simon Msuva, Asad Ally/Mange Gugah/TUmain Venance na Mussa Kanyaga.