Timu ya Azam Academy imeingia hatua ya nusu fainali ya michuano ya Uhai 2011 baada ya kuifunga Moro United kwa penati ya 4-1, katika mchezo wa robo fainali uliochezwa leo kwenye uwanja wa Azam Chamazi. Mchezo huo ulimalizika kwa timu zote kutoka sare ya 1-1, na kupelekea hatua ya kupiga matuta ili kupata mshindi atakayecheza nusu fainali. Azam inayoundwa na wachezaji walio chini ya miaka 17 walianza kupata goli dakika ya 8 ya mchezo huo kupitia kwa Simon Msuva aliyemchambua kipa wa Moro Hashim Nzota na kupiga shuti lililotinga moja kwa moja wavuni. Kipindi cha pili dakika ya 51, Jerome Lambele aliisawazishia Moro United na kupelekea timu zote kumaliza muda kwa sare ya 1-1. Katika mikwaju ya penati, kipa wa Azam Aishi Mfula alikuwa kinara kwa kupangua penati mbili za Moro United, huku wapiga penati za Azam wote walipata. Mikwaju ya Azam ilipigwa na Jafary Mgaya, Kelvin Idd, Eliminus Ryeyna na Mussa Kanyaga wakati penati pekee ya Moro ilipigwa na Awadh Salum. Kwa matokeo hayo Azam FC itakutana na Serengeti Boys (U17) kwenye mchezo wa nusu fainali, Serengeti wametinga nusu fainali baada ya kuifunga Villa Squad 3-0, katika mchezo mwingine Simba nayo imeingia hatua hiyo kwa kuifunga JKT Oljoro 5-2. Mchezo kati ya Azam FC na Serengeti Boys umepewa jina la Azam A vs Azam B kutokana na ukweli kuwa Serengeti Boys inaundwa na wachezaji watano (5) wa kikosi kinachoanza wa Azam FC. Simba watakutana na Toto Africa katika mchezo wao wa nusu fainali, Toto imeingia hatua hiyo baada ya kuifunga JKT Ruvu 4-3. Hii ni mara ya tatu kwa Azam kucheza nusu fainali ya michuano hii, walicheza nusu fainali za mwaka 2008 na 2009 na kuibuka mabingwa wa miaka hiyo. Kikosi Azam kilichotinga nusu fainali, Aishi Mfula, Braison Nkulula, Mohamed Hussein, Dizana Yarouk, Mgaya Japhary, Eliminus Ryeyna, Mange Gugah/ Tumaini Venance, Ally Kaijage, Kelvin Idd, Gadson Naftari/Mussa Kanyaga na Simon Msuva.]