Timu ya Azam Academy imejiandaa vyema na michuano ya vijana chini ya miaka 20 kwa klabu za ligi kuu 'Uhai Cup 2011' japokuwa inaupungufu wa wachezaji sita waliopo timu ya taifa ya vijana U17 'Serengeti Boys'.

Uhai Cup itaanza kesho Nov 12 na kumalizika Nov 25, mwaka huu itachezwa kwenye viwanja viwili, Uwanja wa Azam Chamazi na Uwanja wa Karume.

Azam Academy watacheza mchezo wa kwanza kesho saa tatu asubuhi kwenye uwanja wa Azam Chamazi dhidi ya Kagera Sugar, mbali na mchezo huo kutakuwa na michezo mingine, Moro United dhidi ya Yanga saa nane na saa kumi Simba watacheza dhidi ya Coastal Union kwenye uwanja huo.

Wakati katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, asubuhi mabingwa watetezi Ruvu Shooting watacheza na JKT Oljoro, mchana JKT Ruvu dhidi ya Polisi Dodoma na jioni Toto African wataikaribisha Serengeti Boys.

Kocha wa Azam Academy, Vivek Nagul ameiambia tovuti ya www.azamfc.co.tz kuwa kukosekana kwa wachezaji hao kumeiathri timu hiyo kwa kuwa wachezaji walioondoka wote hucheza katika kikosi cha kwanza.

“Tumebaki na wachezaji 18 tu ambao watacheza kwenye mashindano hayo, kuwakosa wachezai sita ni pigo kwa timu lakini tutajitahidi kufanya vizuri kwa kuwa wachezaji wote wa Academy wapo vizuri” alise,a kocha Nagul.

Ameongeza kuwa wachezaji wengi walioitwa timu ya taifa ni walinzi ambao ni muhimu kwa timu ya yake, hivyo kutumia wachezai wanaokaa benchi mara nyingi huwa wanashindwa kuhimili kucheza vipindi vyote.

Amesema kutokana na uzito na umuhimu wa mashindano hayo timu yake ilicheza mechi kubwa mbili za majaribio dhidi ya timu ya Jack Academy ya Mbagala Market.

Katika matokeo ya kwanza Azam Academy waliifunga timu hiyo 2-1, na mchezo wa marejeano Azam walipata ushindi wa penati 4-1, timu hizo zilifikia hatua ya penati baada ya kumaliza mchezo huo kwa sare ya 2-2.

Akizungumzia lengo la kufikia mikwaju ya penati, kocha Nagul alisema kwenye mashindano makubwa kama Uhai Cup, timu zinaweza kufikia hatua ya kupiga penati ili kupatikana mshindi hivyo kutumia nafasi hiyo kwa mazoezi kwa timu yake.

Wachezaji wa Azam FC watakao cheza Uhai Cup, Mwalo Hashim Ilunga, Dizana Issa, Mohamed Hussein, Mussa John, Ally Kaijage,Tumaini Venancy, John Chedy, Mange Chagula, Abdul Mgaya, Braison Nkulila, Mwinyi Hamad, Renya Mganyila, Idrissa Kibinda, Ramadhan Mbega Rehani. Asad ally na Kelvin friday.

Michuano hiyo inakutanisha jumla ya timu 15, timu 14 za klabu za ligi kuu na timu ya Taifa ya vijana ya serengeti Boys inacheza kama timu mualikwa, timu hizo zipo katika makundi matatu,. Kundi A lina Ruvu Shooting,JKT Oljoro, Azam FC, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar, kundi B zipo JKT Ruvu, Police Dodoma, Yanga, Vila Squad na Moro United wakati kundi C linaundwa na Simba, Coastal Union, Toto Africa, Serengeti Boys na African Lyon.

Hatua ya makundi inayoanza kesho itakamilika Novemba 19, timu nane zitaingia robo fainali itakayoanza Nov 21, na washindi wa robo fainali watacheza nusu fainali Nov 23, fainali na hatua ya kumtafuta mshindi wa tatu itachezwa siku ya mwisho Nov 25 mwaka huu kwenye uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.