Siku chache kabla ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ya Vodacom VPL, kocha wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kwa mara ya kwanza amemuita kikosini golikipa wa Azam FC, Mwadini Ally kuunda kikosi cha wachezaji 22.

Kikosi hicho cha timu ya Taifa kinajiandaa na mechi ya mchujo wa Kombe la Dunia dhidi ya timu ya taifa ya Chad itakayochezwa Novemba 11, N’Djamena nchini Chad.

Mwadini anayetokea kisiwani Zanzibar ameitwa kwa mara ya kwanza kuunda kikosi cha wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mwadini anayecheza kikosi cha timu ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ ameitwa kutokana na kufanya vizuri kwenye mechi za ligi kuu a VPL akiwa amecheza michezo tisa amefungwa magoli mawili tu.

Kikosi hicho kimetangazwa leo asubuhi na kocha Jan Poulsen, timu hiyo itaingia kambini November 3 kwa maandalizi ya mchezo huo na itaondoka wiki ijayo kuelekea nchini Chad.

Katika kikosi hicho jumla ya wachezaji watano kutoka Azam FC wameteuliwa kuunda timu hiyo, wachezaji hao ni Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ na Mrisho Ngassa.

Mchezaji Thomas Ulimwengu anayecheza TP Mazembe nchini DRC ameitwa mara ya kwanza kwenye timu hiyo, wachezaji wengine wanaocheza nje ni pamoja na Idrissa Rajab (Sofapaka, Kenya), Henry Joseph (Kongsvinger IL, Norway), Abdi Kassim na Danny Mrwanda (DT Long An, Vietnam), Mbwana Samata (TP Mazembe), Nizar Khalfan (Vancouver Whitecaps, Canada) na Athuman Machupa (Vasalund IF, Sweden),

Wengine ni Juma Kaseja, Juma Jabu, Juma Nyoso, Shomari Kapombe (Simba), Nadir Haroub, Godfrey Taita, Nurdin Bakari (Yanga) na Shabani Nditi Hussein Javu(Mtibwa Sugar).