Timu ya Azam FC imetoka suluhu na Kagera Sugar katika mchezo wa ligi kuu uliochezwa leo jioni kwenye uwanja wa Kaitaba, mkoani Kagera.

Azam FC na Kagera Sugar zimegawana pointi moja moja, Azam FC imefikisha pointi 22 na kubaki nafasi ya tatu wakati Kagera wao wamefikisha pointi 13 na kupaa hadi nafasi ya 7 kutoka nafasi ya tisa.

Katika mchezo huo timu zote zilicheza kwenye kiwango cha juu, Kagera waliutumia uwanja wao waliouzoea lakini kwa Azam FC uliwapa shida kutokana na sehemu zingine kutokuwa na nyasi.

Azam FC walionekana kupeleka mashambulizi mara kwa mara dakika ya kwanza na 13 Zahor Pazi alishindwa kuifungia timu yake baada ya kupiga mipira iliyotoaka nje.

Kagera  nao walikosa nafasi dakika ya 17, Sunday Frank na dk 70, Themi Felix walikosa nafasi za wazi kwa kupiga mipira iliyookolewa na kipa wa Azam FC, Mwadini Ally.

Ibrahim Mwaipopo alipiga mpira wa adhabu uliogonga mwamba na kurudi uwanjani, Mwaipopo akiwa na viungo Salum Aboubakari, Jabir Aziz, Zahor Pazi na Ramadhan Chombo ‘Redondo’ waliongoza safu ya viungo iliyosumbua Kagera Sugar.

Beki Said Morad alionekana kinara wa safu ya ulinzi kwa kuzuia mashambulizi ya wachezaji wa Kagera Sugar, Moradi aliwapa wakati mgumu wachezaji wa timu hiyo, Moradi alijiunga na Azam msimu huu akitokea Kagera Sugar.

Azam FC walifanya mabadiliko walitoka Jabir Aziz, Zahor Pazi na Ramadhan Chombo ‘Redondo’ nafasi zao zikachukuliwa na Abdulhalim Humud, Kipre Tchetche na Khamis Mcha, Kagera waliingia Juma Mpola na Hussein Swed kuchukua nafasi za Paul Ngwai na Ibrahim Mamba.

Kocha wa Azam FC, Stewart Hall amesema mechi ilikuwa ngumu kwa timu zote, timu yake imecheza katika kiwango cha kawaida imepata nafasi nyingi lakini tatizo la umaliziaji limepelekea kupatikana kwa matokeo hayo.

Azam FC itafanya mazoezi kesho asubuhi na jioni wataelekea mkoani Mwanza kwa maandalizi ya mchezo dhidi ya Toto Africa utakaochezwa siku ya Jumatano kwenye uwanja wa CCM Kirumba.

Kikosi cha Azam FC kilichoivaa Kagera Sugar, Mwadini Ally, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Said Morad, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’, Ibrahim Mwaipopo, Jabir Aziz/Abdulhalim Humud, Samih Haji Nuhu, Zahor Pazi/Kipre Tchetche, Ramadhan Chombo 'Redondo’/Khamis Mcha na John Bocco.

 

Kagera Sugar, Andrew Ntara, Jumanne Nade, David Charles, George Kavila, Malegezi Mwangwa, Paul Ngwai, Sunday Frank, Said Dilunga, Ibrahim Mamba, Themi Felix na Freeman Nesta.