Kiungo Ramadhani Chombo ‘Redondo’ leo jioni  ameifungia Azam FC goli la video na la tatu kwa timu yake na kupelekea timu hiyo kupata ushindi wa 3-1 dhidi ya Police Dodoma, kwenye mchezo wa ligi kuu uliochezwa kwenye uwanja wa Azam Chamazi jijini Dar es Salaam.

Matokeo hayo yameipeleka Azam FC nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu ikiwa na jumla ya pointi 21, ikiwa nyuma ya Simba SC inayoongoza kwa kuwa na pointi 24.

Azam FC imepata ushindi huo ambao safari ilianza mapema dakika ya pili, Mrisho Ngassa aliifungia timu hiyo goli la kwanza kwa kupiga mpira uliopita pembeni ya kipa wa Polisi, Agrton Mkwandiko.

Baada ya goli hilo Azam FC waliongeza mashambulizi dakika ya 14 Agrrey Moris alipiga mpira wa adhabu ukagonga mwamba na kurejea uwanjani.

Polisi walitumia muda mwingi kufanya mashambulizi ya kurejesha goli hilo dakika 29 Juma Semsue alipiga shuti likaokolewa na kipa Mwadini Ally wa Azam FC.

Dakika mbili kabla ya kwenda mapumziko, John Bocco alieyeunga krosi ya Erasto Nyoni aliifungia Azam FC kwa mpira wa kichwa ulitikisa nyavu za Polisi na kupeleka timu zote mapumziko Azam FC ikiwa mbele kwa 2-0.

Bocco amefikisha jumla ya magoli 7 ya kufunga sawa na Keneth Asamoah wa Yanga.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko, Polisi walitoka, Kulwa Mfaume, Nassor Muhagama na Bantu Admin nafasi zao kuchukuliwa na Zahor Ismail, Bryton Mponzi na Hamad Kambangwa, Azam FC waliingia Samih Haji Nuhu na Kipre Tchetche kuchukua nafasi za Ibrahim Shikanda na John Bocco.

Mabadiliko hao yalibadili mchezo na kuwa wa kasi, dakika ya 66 Hamad Kambangwa aliipatia Polisi goli la kufutia machozi akitumia uzembe wa viongo na mabeki wa Azam FC.

Goli hilo ni la kwanza kufungwa kwa kipa wa Azam, Mwadini Ally katika mechi saba alizodaka, Mwadini alicheza mechi sita mfulizo bila kufungwa hata goli moja.

Katika mchezo huo wachezaji wa Azam FC upande wa kiungo wakiongozwa na Redondo, Salum Aboubakar Sure Boy, Ibrahim Mwaipopo na Jabir Aziz walitengeneza nafasi nyingi na kutoa mashambulizi mara kwa mara.

Dakika ya 87, Redondo aliufunga kalamu ya magoli kwa kufunga goli la tatu, baada ya kutumia vema mpira wa adhabu uliopigwa na Ibrahim Mwaipopo na kumalizika kwa mchezo Azam FC wakitoka na ushindi wa 3-1.

Baada ya mchezo huo Azam FC inajiandaa na mechi dhidi ya Mtibwa Sugar itakayochezwa uwanja wa Manungu mkoani Morogoro siku ya Jumanne, Octoba 25.

Azam FC, Mwadini Ally, Erasto Nyoni, Ibrahim Shikanda/Samih Haji Nuhu, Said Morad, Aggrey Moris, Ibrahim Mwaipopo, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’, Jabir Aziz, John Bocco/Kipre Tchetche, Mrisho Ngassa na Ramadhan Chombo ‘Redondo’.