Mchezaji chipukizi wa Azam FC, Himid Mao amefurahishwa na matokeo mazuri ya timu yake wakati hayupo lakini wenzake wamesema kurejea kwake kutaongeza nguvu na kuipeleka timu kwenye nafasi nzuri zaidi.

Himid alikuwa mapumziko ya wiki nane akijiandaa na baadaye kufanya mitihani ya kidato cha nne mwaka huu, mitihani iliyomalizika wiki iliyopita.

Akizungumza na tovuti hii Himidi alisema kutokuwepo uwanjani kwa muda huo alitamani sana kurudi kucheza kwa kuwa mpira upo kwenye damu lakini akatimiza wajibu wake wa kufanya mitihani hiyo.

“nimekaa muda mrefu, nilitamani kucheza lakini mitihani ilibana sana na nilihitaji muda mwingi wa maandalizi, nashukuru klabu ilinipa nafasi ya kutosha Mungu akisaidia majibu yatakuwa mazuri” alisema Himid.

Mchezaji huyo aliyekulia kituo cha Azam Academy alisema ligi ya mwaka huu ni ngumu lakini amefurahishwa na kiwango cha wachezaji wa klabu yake kwa kuwa wameshinda mechi nyingi na kuwa katika nafasi nzuri.

Aliongeza kuwa japokuwa timu ipo vizuri, wachezaji wanatakiwa kuongeza juhudi na kufika mbali zaidi hiyo itasaidia kumalizi ligi wakiwa katika nafasi nzuri.

“Tumebaki na mechi nne kumaliza mzunguko huu, tukijipanga na kuongeza nguvu tutashinda mechi zote na kujiweka sehemu nzuri” alisisitiza Himid.