Timu ya Azam FC kesho itashuka kwenye uwanja wa Azam Chamazi kucheza mchezo wake wa 10 wa ligi kuu ya Vodacom VPL dhidi ya Police Dodoma.

Azam FC itacheza mchezo huo ikiwakosa wachezaji walinzi wake Wazir Salum na Nafiu Awudu wanaosumbuliwa na majeraha, lakini watawatumia wachezaji waliorejea mazoezini Himid Mao, Obren Curcovic na Jabir Aziz.

Akilonga na tovuti ya www.azamfc.co.tz kocha mkuu wa Azam FC, Stewart Hall amesema timu iko vizuri, kurejea kwa wachezaji hao kumeongeza hari na nguvu kwa timu.

“Mechi ya kesho ni ngumu, wachezaji waliopo wanafanya mazoezi na kufanya vizuri, hivyo matokeo yoyote yanaweza kutokea” alisema Stewart.

Kocha Stewart amesema Obren ameanza mazoezi na timu hivyo kesho atakuwa goli kipa namba mbili na golini atakaa kipa Mwadini Ally.

Alisema Jabir amemaliza adhabu aliyokuwa anaitumikiwa kwa kuwa alikuwa na kadi za njano tatu, na Mao ameshamaliza mitihani ya kidato cha nne atakuwepo katika mchezo huo.

Kocha ameongeza Haji Nuhu atakuwepo kwenye kikosi cha kesho kwa kuwa alionyesha kiwango kizuri mchezo uliopita, lakini Abdulghan Ghulam bado anaendelea kufanya mazoezi ya taratibu.

Stewart amewataka wachezaji wa kikosi hicho kujituma zaidi katika mechi zilizobaki ili kumaliza mzunguko wa kwanza wakiwa katika nafasi nzuri.

Azam FC itashuka kwenye mchezo huo ikiwa haijafungwa mechi mechi saba mfululizo ina pointi 18 na kuwa ya tatu katika msimamo wa ligi, wakati Police Dodoma wana pointi 9 wapo katika nafasi ya 11 katika msimamo wa ligi.