Mchezaji Mrisho Ngassa ameifungia Azam FC goli lake la kwanza katika ligi kuu msimu huu na kupelekea timu hiyo kutoka na ushindi wa 2-0 dhidi ya JKT Ruvu, mchezo uliochezwa leo kwenye uwanja wa Azam Chamazi, jijini Dar es Salaam.

Tukio muhimu leo lilikuwa kurejea uwanjani kwa Haji Samih Nuhu, Beki wa kushoto ambaye amekuwa majeruhi kwa muda mrefu sana na leo alirejea na kucheza kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza.

Azam FC wamefikisha ponti 18 kwenye msimamo wa ligi kuu na kupaa hadi nafasi ya tatu, Ngassa alifunga goli hilo sekunde ya 36 ikiwa ni moja magoli ya mapema kufungwa kwenye ligi kuu inayoendelea.

Ngassa aliandika goli hilo baada ya kupokea mpira kutoka kwa Ramadhan Chombo Redondo na kumpiga chenga kipa wa JKT Ruvu Shaaban Dihile na kupiga shuti lililotinga moja kwa moja wavuni.

Goli hilo la mapema liliamsha nguvu kwa JKT ambao walifanya mashambulizi ya nguvu ambapo dakika ya 42 Hussein Bunu alipiga shuti likaokolewa kwa ustadi na kipa wa Azam FC, Mwadini Ally. na kupeleka timu hizo mapumziko Azam FC ikiongoza 1-0.

Kipindi cha pili Azam FC walifanya mabadiliko ambapo walitoka, Abdulhalim Humud na Haji Nuhu nafasi zao zikachukuliwa na Zahor Pazi na Ibrahim Shikanda mabadiliko hayo yaliimarisha kikosi cha Azam FC na kuwafanya warudi mechezoni na kuwamiliki JKT Ruvu. Dakika za 46 na 52 Zahor Pazi alikosa nafasi za wazi kwa kupiga mashuti yalitoka nje na moja kuokolewa na kipa wa JKT Ruvu Shaabani Dihile.

JKT Ruvu walifanya mabadiliko walitoka George Minja, Nashon Naftari na Haruna Adolf nafasi zao kuchukuliwa na Charles Timoth, Jimmy Shoji na Alhaji Zege.

JKT Ruvu walikosa nafasi ya wazi dakika ya 75, Nashon Naftari alibaki yeye na goli lakini alipiga mpira nje ya goli.Kabla ya mpira kumalizika, mshambuliaji John Bocco wa Azam FC alifikisha goli lake la sita baada ya kufunga goli safi kwa kichwa akimalizia kazi nzuri ya Zahoro Pazi.

Bocco amefikisha idadi hiyo ya magoli mengi yakiwa ya kichwa, huku kipa Mwadini akibaki kuwa golikipa pekee kwenye ligi kuu ambaye hajafungwa hata goli moja ambapo leo amefikisha dakika 540.

Katika mchezo wa leo, viungo wa Azam FC wakiongozwa na Ibrahim Mwaipopo na Salum Aboubakar 'Sure Boy' walicheza katika kiwango cha juu na kuwafunika kabisa JKT Ruvu hasa kipindi cha pili, hali hiyo ilipoteza muelekeo kwa timu ya JKT Ruvu ambao muda mwingi waliutumia kulinda goli.

Kocha wa Azam FC Stewart Hall amesema kiwango cha wachezaji wake kimezidi kuhimirika kwa kuwa JKT Ruvu ni timu nzuri na imeonyesha kiwango kizuri hasa kwa kipindi cha kwanza.

Akizungumzia goli la Ngassa kocha amesema mchezo wa leo ulikuwa mzuri kwake, ameweza kufunga mapema na kukosa nafasi nyingi.

Azam FC, Mwadini Ally, Erasto Nyoni, Haji Nuhu/Shikanda, Said Murad, Aggrey Morris, Abdulhalim Humud/Zahor Pazi, Salum Aboubakar, Ibrahim Mwaipopo, John Bocco, Mrisho Ngassa/Kipre Tchetche na Ramadhan Chombo.

JKT Ruvu Shaaban Dihile, Kessy Mapande, Stanley Nkomola, Shaibu Nayopa, Damas Makwaya, George Minja, Nashon Naftari, Haruna Adolf, Hussein Bunu, Rajab Chau na Emanuel Linjechele.