Timu ya Azam FC leo imetoka sare ya 1-1 na Simba SC katika mchezo wa kirafiki uliochezwa kwenye uwanja wa Azam Chamazi jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo ulikuwa ni wa kujipima na kujiweka sawa kwa timu zote, Azam FC waliutumia mchezo huo kama sehemu ya kuwapa uzoefu wachezaji hasa wale wasiopata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.

Wachezaji hao walionyesha kiwango cha juu na kumridhisha kocha mkuu wa klabu hiyo Stewart Hall aliyesema, kiwango cha wachezaji wake kimeongezeka.

“Nimewaona wamecheza vizuri wameshambulia vizuri na walinzi wamefanya kazi nzuri pia viungo walionekana kuhimili mchezo nyakati zote,” alisema Stewart. Hakika Abdulhalim Humud amenifurahisha sana leo.

Kocha ameridhishwa na wachezaji hasa Zahor Pazi aliyefunga goli la kusawazisha dakika 59, Malika Ndeule na Luckson Kakolaki na Abdulhalim Humud.

Katika mchezo huo Simba SC walikuwa wa kwanza kupata goli lililopachikwa wavuni na mchezaji Emmanuel Okwi katika dakika ya tano na kwenda mapumziko Simba ikiongoza 1-0.

Kipindi cha pili Azam FC walianza mpira kwa kasi na kutoa mashambulizi mara kwa mara yaliyozaa matunda katika dakika ya 59 kwa kusawazisha goli lililofungwa na Pazi.

Azam FC waliendelea kuliandama lango la Simba na kupata penati katika dakika ya 61 baada ya mchezaji wa Simba, Jerry Santo kumwangusha Khamis Mcha wakati akijaribu kufunga katika eneo la penati, Mcha aliamua kupiga penati hiyo lakini alipiga shuti lililopita juu ya goli, hivyo kumaliza mchezo kwa timu zote kutoka sare ya 1-1.

Sare hiyo inakuwa ya pili kwa timu hizi ndani ya mwezi mmoja, Azam na Simba zilitoka suluhu katika mchezo wa ligi kuu uliochezwa mwezi uliopita kwenye Uwanja wa Taifa.

Katika mchezo wa leo mshambuliaji Kipre Tchetche alicheza kipindi kifupi ikiwa ni sehemu ya kuanza mazoezi madogomadogo kutokana na kuwa nje ya uwanja kwa wiki mbili kutokana na kusumbuliwa na mauvivu ya nyama za mapaja.

Akizungumzia hali ya Kipre, kocha Stewart alisema mchezaji huyo leo ameanza mazoezi ya taratibu kwa kucheza dakika 15 za mwisho kama kama alivyotakiwa na daktari, hivyo mchezo ujao atacheza dakika zisizozidi 20 hadi itakapokuwa tayari atarejea kucheza kwa kama kawaida.

Kabla ya kuanza mchezo huo ulitanguliwa na vikosi vya vijana vya timu hizo ambao Simba U20 walipata ushindi wa 3-0 dhidi ya Azam Academy U17.

Azam FC: Mwadini Ally, Ibrahim Shikanda, Luckson Kakolaki, Inrahim Mwaipopo, Nafiu Awudu/Said Morad, Wazir Omary/Malika Ndeule, Khamis Mcha/Kipre Tchetche, Jamal Mnyate/Abdulhalim Humud, Salum Aboubakar na Haji Nuhu/Wahab Yahya.