Wakiwa katika maandalizi ya kucheza na JKT Ruvu, Azam FC kesho asubuhi watacheza na Simba SC kwenye uwanja wa Azam Chamazi, jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo ni muhimu kwa timu zote, utazikutanisha timu hizo zikiwa pungufu kwa wachezaji wao kuwepo kwenye timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars'.

Kocha msaidizi wa Azam FC, Kali Ongala amesema mchezo huo ni sehemu ya maandalizi ya ligi kuu na utawapa nafasi wachezaji wasiocheza kujipima.

“Mechi itakuwa sehemu ya maandalizi kwa mechi zijazo, tutatumia kuwapa uzoefu wachezaji wanakaa benchi kwa kuwa wengine wapo timu ya taifa” alisema Kali.

Kali aliongeza kuwa mchezo huo ulipangwa kuchezwa Ijumaa au Jumamosi lakini kocha mkuu wa Azam FC, Stewart Hall aliomba usogezwe hadi jumatatu kwa kuwa timu haiwezi kucheza mechi yeye asipokuwepo, kocha Stewart anatarajiwa kuwasili nchini kesho Jumapili akitokea kwao nchini Uingereza.

Azam FC watacheza mechi ya tisa dhidi ya JKT Ruvu siku ya Jumamosi ijayo kwenye uwanja huo huku Simba wao watacheza na African Lyon siku ya Jumapili ya wiki ijayo.

Akizungumzia hali ya wachezaji, Kali alisema wachezaji wote wapo vizuri na waliokuwa majeruhi wamesharejea isipokuwa Kipre Tchetche anayetarajiwa kuanza mazoezi mepesi siku ya Jumatatu kutokana na kusumbuliwa na nyama za mapaja.

 

Mwisho.

 

Gulam majeruhi yamtesa,

 

 

Mchezaji Abdulghan Gulam Abdallah wa Azam FC, amesikitishwa na kitendo cha kukosa mechi za ligi kuu kutokana na kupata majeraha siku chache kabla ya kuanza kwa ligi hiyo.

Gulam alipata ufa katika kidole gumba cha mguu wa kulia wakati wa maandalizi ya ligi kuu msimu huu na kupelekea kuwa nje ya uwanja wa zaidi ya miezi miwili na nusu.

Akizungumza na tovuti ya www.azamfc.co.tz Gulam alisema kutocheza muda wote huo kumempa unyonge kwa kuwa alihitaji kuonyesha uwezo wake pamoja na kutoa mchango katika timu yake.

“Kutocheza hata mechi moja kunanisononesha kila wakati na kufanya niwe mnyonge, nimeathirika kisaikoligia kwa kuwa timu imeshacheza mechi nane na sijacheza hata moja kutokana na maumivu yanayonikabili” alisema Gulam.

Gulam aliongeza kuwa kwa sasa hali yake inaendelea vizuri, ameshaanza mazoezi takribani wiki tatu zilizopita lakini bado anasikia maumivu kwa mbali yanayopongua kidogo kidogo.

Akielezea kurejea uwanjani Gulam alisema, anaamini kiwango chake hakijashuka hivyo atakaporejea uwanjani uwezo wake utakuwa mzuri na kutoa mchango wake kwenye timu, endapo ataendelea vizuri anatarajia kurejea uwanjani wiki mbili zijazo.

Akizungumzia ligi inayoendelea alisema ligi ni ya ushindani kila timu imejiandaa hivyo wachezaji wanatakiwa kujituma zaidi ili kupata ushindi.

Gulam amesajiliwa akitokea kwenye Klabu ya Malindi ya visiwani Zanzibar lakini tangu asajiliwe hajacheza hata mechi moja ya ligi kuu ya Tanzania bara kutokana na jeraha hilo.