Wakiwa katika maandalizi ya kucheza na JKT Ruvu, Azam FC kesho asubuhi watacheza na Simba SC kwenye uwanja wa Azam Chamazi, jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo ni muhimu kwa timu zote, utazikutanisha timu hizo zikiwa pungufu kwa wachezaji wao kuwepo kwenye timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars'.

Kocha msaidizi wa Azam FC, Kali Ongala amesema mchezo huo ni sehemu ya maandalizi ya ligi kuu na utawapa nafasi wachezaji wasiocheza kujipima.

“Mechi itakuwa sehemu ya maandalizi kwa mechi zijazo, tutatumia kuwapa uzoefu wachezaji wanakaa benchi kwa kuwa wengine wapo timu ya taifa” alisema Kali.

Kali aliongeza kuwa mchezo huo ulipangwa kuchezwa Ijumaa au Jumamosi lakini kocha mkuu wa Azam FC, Stewart Hall aliomba usogezwe hadi jumatatu kwa kuwa timu haiwezi kucheza mechi yeye asipokuwepo, kocha Stewart anatarajiwa kuwasili nchini kesho Jumapili akitokea kwao nchini Uingereza.

Azam FC watacheza mechi ya tisa dhidi ya JKT Ruvu siku ya Jumamosi ijayo kwenye uwanja huo huku Simba wao watacheza na African Lyon siku ya Jumapili ya wiki ijayo.

Akizungumzia hali ya wachezaji, Kali alisema wachezaji wote wapo vizuri na waliokuwa majeruhi wamesharejea isipokuwa Kipre Tchetche anayetarajiwa kuanza mazoezi mepesi siku ya Jumatatu kutokana na kusumbuliwa na nyama za mapaja.