Nimekaa jukwaa kuu la uwanja wa Mabatini mlandizi, naangalia mechi kati ya Azam FC na Ruvu Shooting Stars, Ramadhan Chombo Redondo anapiga mpira na Bocco anafunga goli safi lakini kwa mshangao wa wengi mwamuzi anakataa goli, mpira unaenda goli la Azam FC wachezaji watatu wa Ruvu wapo offside lakini mwamuzi anapeta, ujasiri wa kipa Mwadini Ally unawaokoa Azam FC harafu mpira unarudi kwenye goli la Ruvu JKT, Mrisho Ngasa anafanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari laini mwamuzi  anapeta tena, Ghafla jirani yangu mmoja anasema, hivi maamuzi kama haya ya dhuluma anayofanyiwa Azam FC kama ingekuwa anafanyiwa Simba au Yanga je tungepona hapa? Watu wote kwa pamoja wanajibu “uwanja ungechomwa moto” mwisho wa kunukuu.

Tatizo la waamuzi kukokuwa makini linaharibu mpira wa Tanzania na itachukua muda mrefu kufikia malengo ya kuendeleza soka, kauli hiyo imetolewa na kocha wa Azam FC, Stewart Hall baada ya kumalizika mchezo wa ligi kuu  kati ya Azam FC na Ruvu Shooting.

Mchezo huo umechezwa leo kwenye uwanja wa Mlandizi mkoani  Pwani timu hizo zilimaliza vipindi vyote na kutoka suluhu.

Katika mchezo huo dakika ya 33 Azam FC walipata goli lililofungwa na John Boco kwa kichwa akiunga mpira wa Ramadhan Chombo ‘Redondo’, mwamuzi Martin Saanya wa Morogoro aliamuru kuwa ni goli isipokuwa mwamuzi wa pembeni alikataa goli hilo hivyo likafutwa.

Kitendo hicho kilizua kutoelewana baina ya wachezaji wa Azam na mwamuzi wa mchezo, hali ya kukataliwa goli hilo kulipoteza ari kwa wachezaji wa Azam FC na kupeleka timu hizo mapumziko zikiwa hazijafungana.

Kipindi cha pili mpira ulibadilika kwa pande zote, wachezaji wa Ruvu Shooting, Kassim Linde,  Seif Abdalah na Abdalah Juma walikosa magoli kwa kupiga mashuti yaliyotua mikononi mwa kipa Mwadini Ally wa Azam FC.

Azam FC walifanya mashambulizi nyakati zote dk 48 Redondo alipoga shuti likaokolewa na kipa Benjamin Nengu wa Ruvu, dakika 53 kulitokea tatizo jingine baada ya Mrisho Ngassa kufunga goli akiwa yeye na kipa na mwamuzi wa mchezo huo Saanya alikataa na kusema sio goli.

Azam FC hawakukata tama wakaendeleza mashambulizi dk 63 Ngassa aliiga shuti lililotoka nje, mchezo huo Azam FC walipata kona 12 wakati Ruvu Shooting walipata kona 6.

Kocha Stewart amezungumzia makosa hayo ya waamuzi kuwa ni sehemu kubwa ya kudidimizi soka la Tanzania kwa kuwa wanatoa maamuzi yanayolenga kushusha kiwango cha mpira nchini.

“Huwa sipendi kuongelea waamuzi lakini nyakati zingine inatokea kutokana na maamuzi mabovu yanayofanywa na waamuzi wa Tanzania, bila kuchukua hatua yoyote hali itandelea na kiwango kitazidi kushuka” amesema  Stewart.

Azam FC baada ya kucheza mchezo wa leo itakuwa na pointi 15, timu itakuwa katika mapumziko ya wiki mbili hadi Octoba 15 itakapocheza na Ruvu Shooting  kwenye uwanja wa Azam, Chamazi jijini Dar es Salaam.

Azam FC, Mwadini Ally, Erasto Nyoni, Waziri Salum, Said Morad, Aggrey Moris, Ibrahim Mwaipopo/Khamis Mcha, Salum Aboubakar, Jabir Aziz, John Bocco, Mrisho Ngassa na Ramadhan Chombo.