“Ushindi lazima” ilikuwa ni kauli ya umoja iliyotolewa na wachezaji wa Azam FC sekunde chache kabla ya kuanza kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Coastal Union uliochezwa leo kwenye uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Azam FC walishinda 1-0.

John Bocco alitimiza kauli hiyo iliyotolewa kwa sauti ya pamoja  dakika ya 33 alipofunga goli pekee katika mchezo huo.

Bocco alifunga goli lake la tano katika ligi kuu, baada ya kupiga penati iliyookolewa na kipa wa Coastal, Omari Hamis na kurudi uwanjani ndipo Bocco alirudisha mpira wavuni kwa kichwa.

Penati hiyo ilitolewa baaada ya beki wa Coastal Said Swed kumwangusha Bocco katika eneo la penati, mda mchache baada ya goli hilo Swed aliyekuwa mchezaji wa zamani wa Azam FC alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Omari Maligwa.

Azam FC wameendeleza ushindi, huu ukiwa ushindi wa tatu mfululizo, katika mchezo wa leo timu zote zilianza mchezo wa kasi na kushambuliana kwa kuviziana.

Coastal walitumia muda mwingi kufanya mashambulizi lakini hayakuweza kuandika goli lolote, wachezaji Daniel Lianga, Francis Busungu na Benard Mwalala walikosa magoli kwa kupiga mashuti nje na mengine kuokolewa na kipa mahiri Mwadini Ally.

Mwadini amedhihirisha umahari wake kwa kuokoa mkwaju wa penati ulipogwa na Sabri Mzee ‘China’ wa Coastal Union dk 67, na kuzima ndoto za Coastal kusawazisha goli hilo.

Penati ya Coastal ilisababishwa na beki wa Azam FC, Said Morad aliyemwangusha mshambuliaji Mwalala katika eneo la hatari, kuokolewa kwa penati hiyo kunaweka rekodi kwa kipa Mwadin ya kutofungwa goli hata moja katika michezo minne ya ligi kuu aliyocheza.

Mabadiliko Azam FC walitoka Jabir Aziz na Wahab Yahya nafasi zao kuchukuliwa na Ibrahim Shikanda na Zahor Pazzi mabadiliko hayo yaliongeza kasi kwa Azam FC na kuimarisha safu ya ulinzi iliyozuia mashambulizi ya coastal Union.

Baada ya mchezo kocha wa Azam FC, Stewart Hall alisema tatizo la ubovu wa uwanja wa Mkwakwani umeelekea timu yake kucheza katika kiwango cha chini tofauti na mechi zilizopita.

“Uwanja uliwakosesha wachezaji uwezo wa kucheza katika kiwango kinachotakiwa, lakini matokeo yalikuwa muhimu sana kwetu na tumefanikisha hilo, sasa tunasahau na kujipanga kwa michezo ijayo” alisema Stewart.

Azam FC, Mwadini, Erasto Nyoni, Wazir Salum, Said Morad, Aggrey Moris, Ibrahim Mwaipopo, Salum Abobakari ‘Sure Boy’, Jabir/Shikanda, John Bocco, Wahab/Pazi na Ramadhan Chombo ‘ Redondo’.

Mwisho