Mpira dakika 90 ilikuwa ni kauli ya wapenzi wa soka walioshuhudia Azam FC ikimfunga bingwa mtetezi wa ligi kuu klabu ya Yanga 1-0, katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Azam FC wamepata pointi tatu za nyumbani kupitia goli pekee lililowekwa wavuni na mshambuliaji hatari nchini John Bocco katika dakika ya 20 akiunga pasi ya kupenyeza aliyopokea kutoka kwa kiungo Ibrahim Mwaipopo. Bocco kabla ya kufunga alimchambua golikipa wa Yanga Yaw Berko kasha akafunga kirahisi.

Ushindi huo kwa Azam FC umeamsha matumaini ya mashabiki wake ya kuendelea na safari ya kusaka ubingwa wa ligi kuu kwa msimu wa 2011/2012.

Katika mchezo wa leo Azam FC walikuwa chini ya nahodha msaidizi Aggrey Morris walianza mashambulizi mapema ambapo dakika ya 10 Ramadhan Chombo ‘Redondo’ alikosa goli kwa kupiga mpira wa adhabu ndogo uliotoka nje na dakika 16 Mrisho Ngassa naye alipaisha mpira akiwa yeye na kipa wa Yanga Yaw Berko.

Yanga walikuwa na matumaini ya kushinda mchezo huolakini mpira ni dakika 90, baada ya kupatikana kwa goli hilo la Bocco, Yanga waliamka na kuanza mashambulizi, walifanya mabadiliko ya mapema alitoka Davies Mwape akaingia Kenneth Asamoah lakini hawakubadilisha matokeo na timu kwenda mapumziko Azam wakiongoza 1-0.

Wachezaji wa kiungo Azam FC, Mwaipopo, Redondo, na Jabir Aziz walioneka mwiba kwa viungo wa Yanga baada ya kukatisha safari za Yanga kwa muda wote, huku walinzi  Erasto Nyoni, Said Morad, Wazir Salum na Aggrey wakifunika kwa  ufundi na nguvu kiasi cha kuwafanya washambuliaji wa Yanga waonekane si lolote wala chochote.

Golikipa wa Azam FC leo kwa mara nyingine tena amedhirisha umahiri wake kwa kuokoa hatari zote zilizoelekezwa langoni mwake kwa ufundi mkubwa.

Mwadini amekuwa kipa bora kwa Azam FC, amecheza mechi tatu bila kufungwa, anaonesha kujiamini sana lakini pia tuna Obren Cuckovic ambaye ana kiwango kizuri sana na uzoefu. Kimsingi hatuna tatizo la golikipa amesema kocha wa Azam FC Stewart Hall akijibu Swali la “ameonaje kiwango cha Mwadini”.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko Azam walitoka Bocco, Ngassa na Khamis Mcha wakaingia Zahor Pazi, Ibrahim Shikanda na Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ mabadiliko hayo yaliongeza uwezo wa timu kwa wachezaji kucheza kandanda safi , Yanga walitoka Pius Kisambale na Shamte Ally wakaingia Rashid Gumbo na Godfrey Taita lakini hawakuweza kubadilisha matokeo hayo.

Kocha wa Azam FC, Stewart Hall amesema amefurahishwa na matokeo hayo kwa kuwa wachezaji hawakuonyesha tofauti kutokana na mshambuliaji wake Kipre Tchechte kupata majeraha akiwa mazoezini.

“wamepigana hadi mwisho wa mchezo, kipindi cha kwanza timu ilicheza vizuri sana, lakini kipindi cha pili walionekana kuridhika na matokeo, walinzi wameendelea kufanya vizuri” amesema Stewart.

Kwa matokeo hayo Azam FC imefikisha pointi 11 na kushika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi kuu ikiifuata Simba yenye pointi 14, huku Yanga wakiwa na pointi zao sita.

Azam Mwadini Ally, Erasto Nyoni, Wazir Salum, Said Morad, Aggrey Morris, Ibrahim Mwaipopo, Ramadhan Chombo, Jabir Aziz, John Bocco/Zahor Pazi, Mrisho Ngassa/Ibrahim Shikanda, Khamis Mcha/Salum Aboubakar.

Yanga, Yaw Berko, Shamte Ally, Oscar Joshua, Bakar Mbegu, Shadrack Nsajingwa, Chacha Marwa, Hamis Kiiza, Davies Mwape, Nurdin Bakar na Haruna Niyonzima.