Mchezaji Kipre Tchetche ambaye kwenye mechi za majaribio alikuwa akifunga magoli mazuri kila mechi lakini ghafla magoli yake yalipotea tangia kuanza kwa ligi kuu ya Vodacom leo amefunguka na kumaliza ukame wa magoli baada ya kuiwezesha timu hiyo kupata ushindi wa 2-0 dhidi ya Villa Squad katika mchezo wa ligi kuu uliochezwa leo kwenye uwanja wa Azam, Chamazi  jijini Dar es Salaam.

Baada ya ushindi wa leo Azam FC imefikisha pointi 8 na kupishana pointi mbili na Simba inayoongoza ligi wakiwa na pointi 10, na kuwaacha Villa wakibaki na pointi 4.

Katika mchezo wa leo Kipre Tchetche alifunga goli lake la kwanza tangu aanze kucheza ligi kuu ya Tanzania, na goli la kwanza katika mchezo huo akitumia vyema kosa la kipa wa Villa Squad, Abbas Nassor kuutema mpira uliorudi uwanjani na kukutana na Kipre aliyesogeza wavuni.

Tcheche aliyeonekana mwiba kwa mabeki wa Villa leo katika dakika ya 35 alipiga krosi safi iliyounganishwa kwa kichwa na John Bocco kuandika goli la pili.

Magoli hayo ya kipindi cha kwanza yaliamsha juhudi kwa Villa za kutaka kusawazisha wakiongozwa na mchezaji Mohamed Kijuso ambaye alicheza vizuri kama mshambuliaji wa mwisho leo. Kijuso alipiga shuti likaokolewa na kipa wa Azam FC, Mwadini Ally na Haruna Shamte aliwakosesha goli la kufutia machozi baada ya kupiga mpira wa adhabu uliotoka nje dakika saba kabla mpira kumalizika.

Safu ya ulinzi ya Azam FC imeendelea kuimarika ambapo leo washambuliaji wa Villa hawakupata nafasi kabisa ya kumsumbua kipa Mwadini na kuhakikisha wanapata pointi tatu za ugenini (Azam FC leo ilikuwa ugenini licha ya mchezo kuchezwa Chamazi).

Villa walifanya mabadiliko kuimarisha timu yao walitoka Ahmed Mkweche na Edward Kashamla nafasi zao kuchukuliwa na Ally Bilali na Luseke Kiggi, mabadiliko hayo yalileta uhai kwa Villa lakini hawakuweza kubadili matokeo hayo.

Azam FC walitoka wafungaji wa mchezo huo Kipre na Bocco nafasi zao kuchukuliwa na Zahor Pazi na Wahab Yahaya.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo kocha wa Azam FC, Stewart Hall alisema timu yake imepata ushindi lakini wachezaji hawakucheza katika kiwango kinachostahili.

“tumepata ushindi, wachezaji wamecheza vizuri lakini sio katika kiwango cha juu, nashukuru tumepata pointi tatu, nitaongeza mazoezi zaidi ili tuwe katika nafasi nzuri” alisema Stewart.

Azam FC, Mwadini Ally, Erasto Nyoni, Waziri Salum, Aggrey Morris, Ibrahim Mwaipopo, Ramadhan Chombo, Jabir Aziz, John Bocco/Zahor Pazi, Kipre Tchetche/Wahab Yahaya na Khamis Mcha.