Zilikuwa ni dakika 90 za kandanda safi lililoonyeshwa na Azam FC na kumalizika kwa sare ya bila kufungana dhidi ya Simba SC katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom uliochezwa leo jioni kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Picha juu ni ya mchezaji nyota wa mechi ya jana Ramadhani Chombo Redondo. picha hii ilipigwa kwenye mechi kati ya Azam FC na Moro United iliyofanyika Chamazi Stadium

Azam FC wakiwa nyumbani walizitumia dakika hizo kujaribu kupata ushindi lakini hali ilikuwa tofauti na kupelekea kugawana pointi moja na mabingwa hao wa zamani wa ligi kuu, Azam FC imefikisha pointi 5 huku Simba ikifikisha na pointi 10.

Katika mchezo huo Azam FC walionekana kuwa bora katika idara zote kuanzia golikipa hadi wachezaji wa ndani huku wachezaji wake wakimiliki mchezo kwa dakika zote za mchezo wakitengeneza zaidi ya nafasi sita lakini bahati haikuwa upande wao.

Uwezo mkubwa wa walinzi wa Azam ukiongozwa na nahodha Aggrey Morris na Said Moradi ulionekana kuwafunika Simba kiasi kwamba vijana hao wa Msimbazi hawakuweza kupata nafasi yoyote leo.

 Viungo Ibrahim Mwaipopo, Jabir Aziz na Ramadhan Chombo leo waliwapoteza kabisa akina Mutesa Mafisango na Jerry Santo wa Simba. washambuliaji wakiongozwa na Kipre Tchetche na Bocco walifanya kazi yao vizuri sana lakini bahari haikuwa yao.

Azam FC walikosa nafasi kipindi cha kwanza dakika ya 45, baada ya John Bocco kupiga shuti lililotoka njekipindi cha pili dk 73 walipata mpira wa adhabu uliopigwa na Ibrahim Mwaipopo na kugonga mwamba, wachezaji Kipre, Wahab Yahya na Mrisho Ngassa walipeleka mashambulizi mara kwa mara kwenye lango la Simba mashabulizi ambayo yaliwaweka mashabiki wa simba roho juu muda wote wa mchezo.

Simba wakiwa na timu kamili walitumia nguvu za ziada kulinda lango lao, na kutoa mashambulizi ambayo hayakuzaa matunda, Gervas Kago katika kipindi cha kwanza alipata nafasi mbili lakini alipiga mipira yote nje, Ulimboka  Mwakingwe na Haruna Moshi ‘Boban’ hawakuonekana kuwa na madhara kwa golikipa Mwadini Ally wa Azam FC.

Katika mchezo wa leo Simba walifanya mabadiliko alitoka Amri Kiemba akaingia Shija Mkina lakini akatolewa na kuingia Uhuru Seleman, wakati Azam FC alitoka Kipre Tchetche na kuingia Wahab Yahya.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo, kocha wa Azam FC, Stewart Hall alisema tatizo la umaliziaji limepelekea kupatikana kwa matokeo hayo, kwa kuwa timu yake ilipata nafasi nyingi lakini walishindwa kumalizia.

“Mchezo ulikuwa mzuri, tunashukuru hatujapoteza mchezo wa leo lakini matokeo haya yametokana na tatizo la umaliziaji kwa wachezaji wangu, wamejitahidi wamebadilika tofauti na mechi za kwanza, nitawapa maandalizi zaidi ili tushinde mechi zijazo” alisema Stewart.

Kikosi cha Azam FC kilichoshuka dimbani leo kiliongozwa na kipa Mwadini Ally, Wazir Salum, Aggrey Moris, Erasto Nyoni, Said Morad, Ibrahim Mwaipopo, Jabir Aziz, Mrisho Ngassa, Kipre Tchetche/Wahab Yahya, Ramadhan Chombo na John Bocco.

Simba SC kilikuwa na Juma Kaseja, Nassor Cholo, Amir Maftah, Jerry Santo, Amri Kiemba/Shija Mkina/Uhuru Seleman, Haruna Moshi, Mutesa Mafisango, Ulimboka Mwakingwe, Juma Nyoso, Victor Costa, Gervas Kago.

Wakati huo huo Azam FC itakwaana na Villa Squad katika mchezo wake wa tano wa ligi kuu siku ya jumanne. Baada ya mchezo wa jana Azam FC ilirejea kambini moja kwa moja kujiandaa na mchezo huo ambao utafanyika katika uwanja wa Azam Chamazi.