Azam FC leo imetoka sare 1-1 na JKT Oljoro katika mechi ya tatu ya ligi kuu ya Vodacom mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Azam FC ambao walikuwa wakitafuta ushindi kwa udi na uvumba walipata goli lao katika dakika ya 40 kipindi cha kwanza kupitia kwa John Bocco aliyemchambua kipa wa Oljoro na kufunga.

JKT oljoro walisawazisha kwa njia ya penati baada ya mlizi wa Azam FC waziri Salum Omar kumuangusha mchezaji wa Oljoro katika harakati za kuokoa mpira. Hii ilitokana na golikipa Obren na Mlinzi Aggrey kugongana wakati wakiwania mpira wa juu na kumpa nafasi mchezaji wa Oljoro.

Azam FC itakwaana na Simba hapo jumapili kwenye uwanja wa Taifa katika mfululizo wa mechi za ligi kuu ya Vodacom.

Taarifa rasmi juu ya mechi dhidi ya Simba toka TFF ipo hapo chini

 

VPL KUCHEZWA UWANJA WA TAIFA (by Boniface Wambura TFF)

Serikali imeruhusu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kutumika kwa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zinazohusu timu za Simba na Yanga. Hata hivyo ruhusa hiyo ni ya mechi mbili kwa wiki.

 

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na klabu za VPL zenye maskani yake Dar es Salaam waliwasilisha tena maombi Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ili kutumia uwanja huo kwa mechi za ligi.

 

Kutokana na uamuzi huo wa Serikali mechi ambazo sasa zitachezwa kwenye uwanja huo ni Ruvu Shooting vs Yanga (Septemba 10), Azam vs Simba (Septemba 11), Simba vs Polisi Dodoma (Septemba 14), African Lyon v Yanga (Septemba 15), Azam vs Yanga (Septemba 18), Yanga vs Villa Squad (Septemba 21).

 

Nyingine ni Yanga vs Coastal Union (Septemba 24), Simba vs Mtibwa Sugar (Septemba 25), Yanga vs Kagera Sugar (Oktoba 14), Simba vs African Lyon (Oktoba 16), Simba vs Ruvu Shooting (Oktoba 19), Yanga vs Toto Africans (Oktoba 20), Simba vs JKT Ruvu (Oktoba 22), Yanga vs Oljoro (Oktoba 23), Yanga vs Simba (Oktoba 29) na Moro United vs Simba (Novemba 5).