Mji wa Arusha umejaa ukungu, hali ya hewa ni baridi kali sana ikiambatana na manyunyu ya mvua. Hali hii si nzuri sana hasa kwa wakazi toka dar es Salaam ambako hali ya hewa ni joto. Webmaster amejifungia chumbani hotelini kwake na akiangalia dirishani kwa nje, kila anayepita barabarani amevaa koti zito. Azam FC imeweka kambi kwenye hoteli ya Aqulline jirani na stendi kuu ikisubiri muda ufike ielekee kwenye uwanja mkongwe na wenye historia kubwa katika soka la nchi yetu. Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kuikabili timu ngumu ya JKT Oljoro.

Kwa mujibu wa ratiba ya leo, dakika 10 zijazo kikao kati ya benchi la ufundi na wachezaji kitaanza. Kikao hiki kitakuwa na ajenda moja tuu ya mikakati ya ushindi. Baada ya hapo wachezaji watapumzika na kupata chakula cha mchana kabla ya kuelekea uwanjani kuvaana na Oljoro.

Azam FC inashika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi yenye timu 14, msimamo ambao unaongozwa na Simba huku Yanga ikishika mkia. Endapo Azam FC itashinda mechi ya leo basi itafikisha pointi sita (6) na kupaa hadi nafasi ya tano. Ikiwa nyuma kwa pointi tatu kwa vinala wa ligi JKT Ruvu na Simba wenye pointi tisa (9) kila mmoja.

Wachezaji wote waliosafiri na timu wapo katika hali nzuri sana wakiusubiri mchezo huu.

Azam FC ambayo ilipoteza mchezo wake uliopita baada ya kufungwa kizembe na African Lyon FC 0-1 inahitaji kwa udi na uvumba ushindi wa leo ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kuwania nafasi mbili za juu za kuwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa.

Akizungumza na tovuti ya Azam FC, kocha msaidizi wa Azam FC kalimangonga Rampling Daniel Ongala AVB amesema kwa maandalizi waliyoyafanya ana uhakika wa kuibuka na ushindi na kujiweka katika mazingira bora ya kuwania taji la VPL msimu huu.

Timu inatarajiwa kuwakilishwa na Obren, Erasto, Waziri, Moradi, Aggrey, Mwaipopo, Ngasa, Jabir, Bocco, Kipre na Chombo.