Kutolewa kwa kadi nyekundu mchezaji Salum Aboubakar 'Sure Boy' wa Azam FC kumepelekea timu hiyo kupoteza mchezo wake wa ligi kuu kwa kufungwa 1-0 na African Lyon, katika mchezo uliochezwa leo jioni uwanja wa Azam jijini Dar es Salaam

Katika mchezo huo Azam FC walitawala kipindi chote cha kwanza lakini haikuwa bahati kwao kupata golikipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko Azam FC walitoka Kipre Tchetche na John Bocco nafasi zao kuchukuliwa na Khamis Mcha na Yahya Wahab.

Mabadiliko hayo yaliongeza kasi ya mchezo huo lakini dakika ya 67 mchezaji wa Lyon Semmy Kessy alimtendea madhambi Sure Boy, Sure alifanya kosa na kumrudishia mchezaji huyo kwa kumpiga kiwiko, ndipo mwamuzi wa mchezo Israel Nkongo wa Dar es Salaam, alimunyesha kadi nyekundu Sure na kumtoa katika mchezo.

Azam FC ikibaki na wachezaji 10 uwanjani walifanya mashambulizi na kulinda goli, Lyon walitumia vyema mapungufu yao katika dakika ya 86 ya mchezo huo, Adam Kingwande aliyeingia kuchukua nafasi ya Kessy aliifungia Lyon goli pekee na la ushindi katika mchezo huo.

Baada ya mchezo kumalizika kocha wa Azam FC, Stewart Hall alisema timu yake imecheza vizuri japo walikuwa na mapungufu ya mchezaji mmoja.

"Kucheza wachezaji kumi kulibadili mchezo, wachezaji walitakiwa kucheza kwa uangalifu zaidi ili kuzuia huku wakifanya mashambulizi, kumkosa Sure kumepelekea kupoteza mchezo wa leo" alisema Hall.

Azam FC imebaki na pointi tatu iliyopata katika mchezo wake wa kwanza wa ligi, baada ya kuifunga Moro United 1-0, huku Lyon wanakuwa na pointi 4 baada ya kutoka sare ya 1-1 na Police Dodoma katika mechi ya kwanza.

Azam FC watacheza mchezo wake wa tatu wa ligi kuu Sept 7 dhidi ya JKT Oljoro, mchezo utakaochezwa jijini Arusha, katika uwanja wa kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid.

Azam FC, Obren Cucovic, Ibrahim Shikanda, Waziri Omary, Awudu Nafiu, Aggrey Morris, Jabir Aziz, Mrisho Ngassa, Sure Boy, John Bocco/Wahab Yahya, Tchetche Kipre/Khamis Mcha na Ramadhan Chombo Redondo.