Ikicheza kandanda safi lililowaacha na mshangao mkubwa watu wa Kampala. Azam FC leo imefanikiwa kutoka sare ya 0-0 na wenyeji SC Villa katika mchezo mkali wa kuvutia uliochezwa kwenye uwanja mkongwe wa Nakivubo.

Azam FC ambayo ipo kwenye mechi za majaribio leo ilijaribu mfumo wake mpya wa kucheza kwenye viwanja vibovu hasa ukizingatia kwenye ligi kuu ya Vodacom ambayo itaanza wiki ijayo kuna mechi zaidi ya sita ambazo tutapaswa kucheza kwenye viwanja vibovu. Viwanja hivyo ni Mkwakwani Tanga, Sheikh Amri Abeid Arusha, Jamhuri Dodoma, JKT Mlandizi na Kaitaba Bukoba huku viwanja vizuri vikiwa Taifa DSM, Azam Stadium Chamazi, Manungu Complex na CCM Kirumba Mwanza.

Said Morrad ambaye timu imemsajili toka Kagera Sugar, Abdul Halim Humud toka Simba na Waziri Salum toka Mafunzo ya Zanzibar leo walikuwa katika kiwango cha juu sana na walig’ara sana. Mwalimu Stewart Hall amesema amefurahishwa sana na kiwango cha timu yake leo hasa upande wa ulinzi na anachohitaji sasa ni kufanyia kazi eneo la ushambuliaji.

Azam FC leo iliwakilishwa na, Mwadini Ally, Erasto Nyoni, Waziri Salum, Said Morrad, Aggrey Morris, Abdulhalim Humud, Jabir Aziz, Ramadhan Chombo, John Bocco, Kipre Tchetche na Mrisho Ngasa

Wakati huo huo Azam FC kesho itashuka kwenye uwanja huo huo wa Nakivubo kukwaana na Kampala City Council katika muendelezo wa mechi zake za kujipima nguvu kambla ya kuanza ligi kuu ya Vodacom.

Kikosi kinachotarajia kuanza kesho ni Obren Cockovic, Ibrahim Shikanda, Malika Philip Ndeule, Aggrey Morris, Nafiu Awudu, Himid Mao, Ibrahim mwaipopo, Salum Abubakar, Wahab Yahaya, Zahoro Pazi na Khamis Mcha Viali