Zahor Pazi na Khamis Mcha wamekamilisha mechi za kirafiki kwa kuipa ushindi wa 2-0 timu ya Azam FC dhidi ya Police Dodoma katika mchezo uliochezwa leo jioni Azam Stadium jijini Dar es Salaam.

Azam FC walicheza mchezo huo kukamilisha mechi za kirafiki kwa timu za ndani ikiwa ni siku mbili kabla ya kuelekea ziarani nchini Uganda na Rwanda kwa ajili ya kucheza mechi za kirafiki za kimataifa.

 Wachezaji wa Azam FC walitumia nafasi hiyo kujipima zaidi kwa kuonyesha uwezo uliowahakikishia kufanya vizuri katika mechi za ligi kuu zinazotarajiwa kuanza August 20 mwaka huu.

Upande wa Police Dodoma huu ulikuwa mchezo wa pili wa maandalizi ya ligi kuu, walianza mchezo huo kwa kucheza kwa kasi huku Azam FC wakicheza kwa mtindo wa pasi nyingi sambamba na mashambulizi.

Kipindi cha kwanza timu zote zilitoka bila kufungana huku mchezaji Kipre Tchetche akionekana kuwapa kazi ya ziada mabeki wa Police Dodoma.

Kipindi cha pili Azam FC waliendeleza kasi baada ya kufanya mabadiliko kwa kuwarudisha benchi  Kipre, Wahab Yahya, Nafiu Awudu na Jamal Mnyate nafasi zao kuchukuliwa na Zahor Pazi, Khamis Mcha, Wazir Salum na Ramadhan Chombo huku Police iliwatoa Elius Mashaka, Briton Mponji na kuwapa nafasi Nassor Muhagama na Abdala Seif.

Mabadiliko upande wa Azam FC yalibadili matokeo kwa Azam FC kupata goli la kwanza dakika ya 56 kwa kichwa kilichowekwa wavuni na Mcha akiunga krosi ya safi ya beki Wazir Salum.

Azam FC baada ya kupata goli hilo walipata nguvu mpya na kuongeza mashambulizi na kuwaacha Police Dom wakitafuta nafasi ya kusawazisha, wakiwa wanatafuta nafasi hiyo Zahor Pazi aliongeza goli la pili dakika ya 74 akiwaacha mabeki na kupiga shuti aina ya ‘Kanzu’ iliyomuacha kipa wa Police Akbir Santu akiwa hana la kufanya na mpira kwenda wavuni moja kwa moja.

Goli la pili liliwapa wakati mgumu Police Dom, waliojaribu kusawazisha lakini muda ukawatupa mkono na kuondoka wakiwa wamepoteza mchezo huo.

Matokeo hayo yanakamilisha safari ya mechi za kirafiki, Azam FC walizifunga Villa 5-0, Ruvu Shooting 1-0, Moro United 3-0, JKT Ruvu 3-2 na Azam Academy 3-2, ikatoka sare na Kombaini ya Majeshi 1-1 na Zanzibar Select 0-0 na kupoteza 2-0  dhidi ya Coastal Union, itaelekea nchini Uganda na Rwanda kwa mechi tano za kirafiki.

Azam FC Mwadini, Nyoni, Malika/Luckson, Salum Aboubakar, Moradi, Mwaipopo/Himid, Kipre/Pazi, Humud, Mnyate/Chombo, Nafiu/Wazir na Wahab/Mcha.