“Dah Ngasa fundi hatari!” yalikuwa ni baadhi ya maneno ya mashabiki waliyotoa baada ya mchezaji Mrisho Ngassa kuipatia Azam FC goli la ushindi katika mchezo wa kirafiki dhidi ya JKT Ruvu uliomalizika kwa Azam FC kuibuka na ushindi wa 3-2.

Ngassa alifunga goli hilo dakika ya 90 kwa tick-tack akiunga krosi ya Ramadhani Chombo Redondo na kuiwezesha Azam FC kuendeleza ushindi katika mechi zake za kirafiki, ikiwa imeshinda michezo minne, sare miwili na kufungwa mchezo mmoja.

Mchezo huo ulichezwa leo jinni Azam Stadium, Chamazi jijini Dar es Salaam, JKT Ruvu walianza kupata goli dakika ya 5 ya mchezo kupitia kwa Amos Mugisa, goli ambalo liliwapa nguvu na kufanikiwa kuongeza goli la pili dakika ya 21 lililofungwa na Hussein Bunu.

Magoli mawili ya haraka yaliwatuliza Azam na kuanza kutafuta nafasi za kurudisha, dakika tatu baadae 'dk 24', Kipre Tchetche alianza kwa kuandika goli la kwanza kiufundi baada ya kuichambua Ngome ya JKT Ruvu iliyokuwa chini ya Nahodha wake Shaibu Nayopa.

JKT Ruvu walianza kujipanga kulinda lango lao lakini hawakufanikiwa kuzuia kasi ya mchezo wa Azam, iliyoongozwa na Kipre, Kipre tena  aliwaacha viungo na walinzi wa JKT kwenye mataa ya feri na akampa pasi John Bocco na kufunga goli la pili kwa Azam FC, magoli hayo yalizipeleka timu zote mapumziko zikiwa 2-2.

Kipindi cha pili timu zote zilionyesha kandanda safi kwa kucheza soka la hali ya juu, kuhu kukiwa na ubabe na rafu za hapa na pale.

Azam FC walipata nafasi nyingi za kufunga kuliko JKT Ruvu ambao muda mwingi walicheza katikati na kutoa mashambulizi machache.

Maafande hao wakiwa na matumaini ya kumaliza mchezo kwa sare ya 2-2, Azam FC walianza kuliandama goli la JKT kwa mashambulizi ya mara kwa mara ndipo Redondo aliachia krosi iliyochezwa vizuri na Ngasa kwa mtindo wa kuruka kwa kijipinda 'tick-tak' na kukamilisha kalamu ya magoli 3-2.

Azam FC itacheza mchezo wake wa nane wa kirafiki dhidi ya Polisi Dodoma ukiwa mchezo mbadala kufuatia Costal Union ya Tanga kuingia mitini ambapo waliomba awali kucheza na Azam FC mchezo wa marejeano baada ya Coastal kushinda 2-0 mchezo uliopita,.

Azam FC imecheza mechi dhidi ya Villa Squad na kuifunga 5-0, Moro United na kushinda 3-0,  kombaini ya Majeshi na kutoka nayo sare ya 1-1, Zanzibar Select na kutoka nayo sare ya 0-0, Azam Academy ambayo ilifungwa 3-2, Coastal Union ambayo iliifunga Azam FC 2-0, na Ruvu Shooting ambapo Azam ilishinda 1-0.

Azam FC, Obren, Shikanda, Agrey, Wazir, Nafiu/Luckson, Mwaipopo/Humud, Jabir/Salum ‘Sureboy’,Bocco/ Zahor Pazi, Kipre/Mnyate,Ngassa