Uwanja wa Azam Stadium uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam unatarajiwa kuchezesha idadi ya mechi 54 za ligi kuu ya Tanzania, VPL itakayoanza August 20 mwaka huu.

Idadi hiyo ya mechi imetokana na timu tano za ligi kuu kuutumia uwanja huo kwa mechi zao za nyumbani kutokana na uwanja wa Uhuru kuwa katika matengenezo.

Hii ni mara ya kwanza kwa uwanja huo wenye nyasi bandia kutumika katika mechi za ligi kuu, Azam Stadium ambao umefikia kiwango cha kutunukiwa hati na FIFA ya kuchezea michezo ya kandanda, ni uwanja wa aina yake kumilikiwa na klabu Afrika Mashariki

Timu za African Lyon, JKT Ruvu, Moro United, Villa Squad na Azam FC zote za Dar es Salaam ziliomba kuutumia uwanja huo kwa mechi zote isipokuwa mechi zitakazocheza na Simba na Yanga kutokana na uwanja huo kutokuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki wengi.

Uongozi wa Azam FC, uliwataka timu zote zilizoomba kuutumia uwanja huo kuainisha kwamba mechi zote za Simba na Yanga zitatakiwa kuchezwa uwanja mwingine ukiwepo uwanja wa Taifa.

Shirikisho la mpira wa Miguu nchini siku ya Jumanne limetoa ratiba yake ya ligi kuu kwa mizunguko yote miwili, ratiba inayoonyesha michezo ya nyumbani ya timu hizo kuchezwa Azam Stadium huku zile za Simba na Yanga zitachezwa uwanja wa Taifa.

Azam Stadium itachezesha jumla ya mechi 54, 25 katika mzunguko wa kwanza na mechi 29 za mzunguko wa pili, huku kila wiki kukiwa na wastani wa mechi mbili, Uwanja wa taifa utakuwa na jumla ya mechi 37.

Mechi za uwanja wa Taifa utakaotumiwa na Simba na Yanga kama uwanja wao wa nyumbani, utajumuisha mechi za African Lyon, JKT Ruvu, Moro United, Villa Squad, Azam FC na Ruvu Shooting zitakazocheza dhidi ya timu hizo.

Viwanja vingine kama Kaitaba wa Kagera(Kagera Sugar), CCM Kirumba wa Mwanza (Toto Africa), Mkwakwani wa Tanga (Coastal Union), Sheikh Amri Abeid wa Arusha (JKT Oljoro) na Jamhuri Dodoma (Police Dodoma) zitatumika kwa idadi ya mechi 13 kila mmoja huku viwanja vya Mlandiz (Ruvu Shooting), Manungu na Jamhuri Morogoro (Mtibwa Sugar) vikiwa na mechi 11.