Kipre Tchetche, mchezaji wa kimataifa toka Ivory Coast leo ameichezea timu yake ya Azam FC mchezo wa kwanza na kuiongoza kuidungua Villa Squad 5-0. Khamis Mcha, Ibrahim Mwaipopo na John Bocco walifunga goli moja kila mmoja huku Kipre akifunga mawili katika ushindi wa 5-0, mchezo huo ulikuwa ni wa kujipima nguvu uliofanyika leo asubuhi uwanjani Chamazi jijini Dar es Salaam.

Azam FC na Villa zimecheza mchezo huo ikiwa ni moja ya sehemu ya matayarisho na kuweka sawa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ya Vodacom unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi ujao.

Mchezo huo ulianza kwa Azam FC kupata goli la kwanza dakika ya kwanza ya mchezo kupitia kwa Hamis Mcha aliyeunga krosi safi iliyopigwa na Kipre Tchetche, goli hilo liliwachanganya wachezaji wa Villa na kuanza kucheza mpira wa kuzuia na kufanya mashambulizi machache.

Wakiwa bado hawajakaa vizuri Ibrahim Mwaipopo akitumia mguu wake wa kushoto aliandika goli la pili dakika ya 32 akimalizia kazi nzuri iliyoanzwa na Jamal Mnyate na kumpa Mcha aliyemtupia kwa Mwaipopo.

Villa walianza kutafakari magoli hayo na kubadilisha mchezo wakitaka kutafuta goli lakini hawakufanikiwa hadi kufikia mapumziko Azam FC walikuwa mbele kwa 2-0.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko machache, mabadiliko hayo yalibadilisha mchezo kwa kiasi kikubwa lakini yakitoa nafasi kwa Azam FC kuandika goli la tatu dakika ya 58 liliwekwa wavuni kwa kichwa cha mshambulia Kipre aliyeunga krosi ya Mcha.

Dakika 10 baadaye Kipre aliongeza goli la nne akimalizia kazi nzuri ya Zahor Pazi aliyeonekana kuisumbua mara kwa mara ngome ya Villa.

Wachezaji wapya wakiwemo Zahor Pazi na Abdul Wahab waliweza kucheza katika kiwango cha hali ya juu pamoja na Nafiu Awudu, Khamis Mcha, Said Moradi na Kipre Tchetche.

Magoli manne ya Azam FC yaliibadilisha Villa na kuanza kucheza mpira wa kutafuta goli wakisahau safu nzima ya ulinzi, hali hiyo ilitoa nafasi kwa mshambulia mahiri John Bocco kutumia wakati huo kuwaacha walinzi wa Villa wakiwa na kipa wao kwa kuachia shuti lililotinga wavuni  na kukamilisha hesabu ya goli 5-0 katika dakika ya 83 ya mchezo.

Baada ya mchezo huo kocha msaidizi wa Villa, Richard Mbuya amesema kipigo hicho kimetokana na kutozoeana kwa wachezaji wazamani na wapya ambao wamesajiliwa kwa ajili ya ligi.

Mbuya ameongeza kuwa kikosi kilichocheza mchezo huo hakikuwa kamili kwani wachezaji wengine wataanza mazoezi siku ya Jumatatu, baada ya hapo wataomba kucheza tena mchezo mwingine wiki zijazo.

Kocha wa Azam FC, Stewart Hall amesema ameridhika na kiwango katika mchezo wa leo japokuwa hakikuwa kikosi kamili, wachezaji Jabir Aziz, Ramadhan Chombo na Mrisho Ngasa na Luckson kakolaki, hawakucheza.

Amesema wachezaji wamecheza kulingana na uwezo wao, wameonyesha maendeleo kadri siku zinavyokwenda na watakuwa wachezaji imara na wazuri.

Azam FC waliocheza leo ni Mwadin Ally/Obrein Cuckovic, Erasto Nyoni/ Ibrahim Shikanda, Malika Ndeule/Waziri Salum, Aggrey Morris/Said Morrad, Nafiu Awudu, Himid Mao/Salum Aboubakar Ibrahim Mwaipopo/Abdulhalim Humud, Kipre/Bocco/Abdul Wahab, Jamal Mnyate/Zahor Pazi.