Kikosi kamili cha Azam FC kimeendelea na mazoezi ya kujenga misuli katika kituo cha mazoezi cha Fitness Masters, wakiwa chini ya kocha wa viungo Jarno Ferikainen kutoka nchini Finland.

Azam FC wanafanya mazoezi ya viungo mara tatu kwa wiki sambamba na mara tatu kwa mazoezi ya uwanjani yanayofanyika Chamazi Complex.

Jarno amelonga na tovuti ya Azam FC na kusema wachezaji wanaendelea vizuri na mazoezi ambayo yanafanyika siku za Jumatatu, Jumatano na Ijumaa kila wiki, yatadumu kwa kipindi chote cha matayarisho kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu.

"wachezaji walianza kwa tabu lakini wameanza kwenda vizuri, iliwapa ugumu mwanzoni kwa kuwa hawakupata mazoezi kama haya hapo nyuma, sasa wametambua umuhimu wa mazoezi ya viungo na wanafanya vizuri kadri siku zinayokwenda." Jarno.

Mtaalam huyo ameongeza kuwa timu itafanya mazoezi ya siku tatu kwa wiki lakini wakati wa ligi watakuwa wakifanya mazoezi hayo mara moja kwa wiki.

Naye kocha mkuu wa klabu, Stewart Hall amesema wachezaji wa kigeni wameanza vyema mazoezi hayo akiwapo Kipre Tche Tche ambaye ameonyesha uwezo mkubwa mazoezini na hata nje ya uwanja kwa kuwa na uhusiano mwema na wachezaji wengine.

"Kipre amekuwa mchezaji mzuri anaelewana na wachezaji wenzake kana kwamba walikuwa wote hapo nyuma, lakini kwa wachezaji wa kutoka Ghana Wahab Yahaya na Nafiu Awudu bado wageni hivyo ni mapema sana kujua mwenendo wao." amesema Hall.

Akizungumzia wachezaji wapya wa hapa nchini amesema wote wameonyesha nidhamu ya hali ya juu na uwezo wao katika mazoezi, anaamini kuwa wachezaji wote watakuwa katika hali nzuri baada ya kukamilika program nzima ya maandalizi ya ligi kuu inayotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi August mwaka huu.

Ameongeza kuwa kabla kuanza kwa ligi timu itaweka kambi ya muda visiwani Zanzibar mwanzoni mwa mwezi August kwa matayarisho ili kubadili mazingira ya mazooezi na hali ya hewa kwa wachezaji.

Azam FC inafanya mazoezi ya kiwanjani siku za Jumanne, Alhamis na Jumamosi, siku za Jumatatu, Jumatano na Ijumaa wanakuwa gym kujenga mwili huku siku ya Jumapili wanapumzika.