Kikosi cha wachezaji 20 wa Azam Academy kinatarajia kuondoka kesho asubuhi kulekea jijini Arusha kushiriki Mashindano ya soka ya Afrika Mashariki na Kati kwa vijana chini ya miaka 20 yanayoandaliwa na Taasisi ya kuibua na kukuza vijana ya Rollingstone.

Azam Academy itaondoka ikiwa na kikosi kilichoandaliwa vyema kwa ajili ya mashindano hayo ya vijana yanayojumuisha timu ishirini, yanatarajiwa kuanza Julai 9 mwaka huu katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Kocha wa vijana Azam Academy, Vivek Nagul amesema wachezaji wamejiandaa vyema kwa mashindanohayo ambayo atayatumia kama sehemu ya kujenga kikosi chake ikiwa ni muda mchache tangu alipochakua wachezaji wapya kuunda timu hiyo.

Amesema wachezaji wengi ni wageni, hivyo mashindano hayo yatakuwa sehemu kubwa ya maandalizi na kufanya usajili sahihi, kwani mchezaji mzuri anaonekana katika mashindano muhimu.

“Timu imejiunga muda mchache, lakini imeweza kufanya vizuri mazoezini, naamini kupitia mashindano hayo itakuwa muda mzuri kujenga timu na kuona uwezo wa wachezaji na kuwaweka pamoja kama timu moja.” Amesema Nagul.

Wachezaji wanaounda Azam Academy ya sasa wamechukuliwa kupitia mashindano ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Copa Coca Cola U17 yaliyomalizika hivi karibuni, wachezaji wanatoka timu mbalimbali kama Kigoma, Mwanza, Ilala na Arusha.

Ameongeza kuwa timu imefanya matayarisho kwa kucheza mechi mbili za kirafiki, ya kwanza iliweza kuifunga timu ya vijana ya IP Sports 10-0 kabla ya kufungwa 3-2 na kikosi cha Azam FC, michezo yote ilifanyika Chamazi Complex.

Katika mchezo dhidi ya Azam FC uliochezwa leo asubuhi, timu zilichezesha wachezaji wote kwa nyakati tofauti, magoli ya Academy yalifungwa na Cosmas Lewis na Ally Kajaige huku Ramadhan Chombo akifunga mawili na Seleman Kassim ‘Selembe’ wakiifungia Azam FC.

Akizungumzia matokeo ya michezo hiyo kocha amesema ni maandalizi mazuri kwa timu, wameonyesha kiwango kizuri, kiwango ambacho anaamini kitajengeka zaidi baada ya kumalizika kwa mashindano hayo.

Azam itaungana na timu zingine za kutoka Kenya, Burundi, Congo, Rwanda na Uganda, huku Tanzania itakuwa na timu za Simba B, Yanga B, Ruvu Shooting B, Oljoro JKT B,  Zanzibar Kaskazini,  Zanzibar Magharibi, Don Breakers, Saadani,  Mbeya Art, Street Children,  Tea, Tanga Yorth, Kong Hearald, Twalipo, Hananasifu, Flamingo, Rollingstone, Jamhuri, CDTI na Bishop Durning.

Kikosi cha Azam Academy kitakacholekea Arusha kitakuwa na wachezaji Hashim Ilunga, Dizana Issa, Adam Mchembi, Mwinyi Hamad, Renya Mganyila, Ally Kaijage, Idrissa Kibinda, Wandwi Willium, Ibrahim Rajab, Mussa John, Omary Mtaki, Mohamed Hussein, Cosmas Lewis, Ismail Adam, Joseph Kimwaga, Abdul Mgaya, Mange Chagula, Ramadhan Mbega, Rehani na Braison Nkulila.