Msimu wa usajili kwa ajili ya ligi kuu ya Tanzania Bara VPL umefunguliwa rasmi hivi majuzi. Sasa vilabu vya ligi kuu vipo bize vikisaka wachezaji watakaovichezea msimu ujao 2011/12. Azam FC ni sehemu ya vilabu hivyo lakini hivi sasa Azam FC haitafuti wachezaji ila inamalizia taratibu za kuwahamisha wachezaji ilyowasajili kwani hadi hivi sasa Azam FC imeshafunga zoezi la usajili.

 

Azam FC imesajili wachezaji 11 wapya na kubakisha 15 wa kikosi kilichomaliza nafasi ya tatu msimu uliopita. Kwa haraka haraka unaweza ukadhani Azam FC imesajili wachezaji wengi wapya na kuacha wachezaji wengi sana wa kikosi kilichopita lakini ukweli ni kwamba Azam FC imeondoa wachezaji katika nafasi mbili tuu. Golikipa na Beki wa kushoto.

 

Ukiangalia kikosi cha Azam FC kilichokuwa kikianza msimu uliopita, utagundua kuwa ukiondoa golikipa ambapo walikuwa wakicheza Jackson Chove na Vladmir Niyonkuru na beki wa kushoto ambako walikuwa wakianza Mau Bofu Ally (raundi ya kwanza) na baadaye Mutesa Patrick Mafisango (raundi ya pili)Azam FC haijaondoa mchezaj hata mmoja wa kikosi cha kwanza msimu huu.

Beki wa kulia na nahodha Ibrahim Shikanda bado yupo. Mabeki wa kati Erasto Nyoni na Aggrey Morris bado wapo. Viungo tegemeo Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo, Salum Abubakar na Ramadhan Chombo Redondo bado wapo na washambuliaji Jamal Mnyate, Mrisho Ngasa na John Raphael Bocco bado wataendelea kuwa tegemeo kwenye kikosi cha Azam FC.

Kuna Swali ambalo uongozi wa benchi la ufundi umekuwa ukikutana nalo mitaani nalo ni ilikuwaje mchezaji mahiri kama Mutesa Patrick Mafisango atolewe kwa Simba na kuchukuliwa mchezaji aliyekuwa akisugua benchi Simba SC Abdulhalim Humud. Jawabu ni rahisi sana, kwanza ikumbukwe kwamba Abdulhalim Humud ameshafundishwa na kocha Stewart Hall kwenye kikosi cha Zanzibar kwa hiyo kocha alipopendekeza tuiombe Simba itupe hata kwa kuwafidia mafisango alikuwa akijua alichokuwa akikifanya.

Pili Azam FC inacheza 4-3-3 ikitumia viungo wawili sehemu ya ukabaji na mmoja mbele yao. Baada ya Stewart Hall kuwatazama kiundani wachezaji wake wote na kuangalia namna ambavyo wata-fit kwenye mfumo wake. Aliona pengo la mchezaji wa aina ya Humud lakini Mafisango ambaye anatumia mguu wa kushoto kama Ibrahim Mwaipopo ilionekana kheri kumtoa ili kumpata mchezaji anayetumia mguu wa kulia kuweza ku-ballance sehemu ya kiungo.

Kuna suala la pili ambalo mashabiki wengi wamekuwa wakiuliza hasa kupitia mtandao wa facebook kuwa Azam FC imejaza Wazanzibari wengi. Stewart Hall anaamini kuwa mwadini Ally Mwadini(kipa wa kimataifa wa Zanzibar) ni bora kuliko makipa wote wa-kitanzania waliokuwa wakicheza ligi kuu ya bara, kutokana na ubora wake ndiyo maana Azam FC ikapanda boti kwenda kumleta.

Baada ya kuondoka Mafisango timu ikabaki na pengo kwenye beki wa kushoto na, ukiangalia ligi kuu ya Tanzania bara, hakuna beki wa kushoto mwenye kimo kizuri, uwezo wa kumiliki mpira na kukaba kumzidi Waziri Salum Omar wa mafunzo ya Zanzibar na ndiyo maana kwenye mashindano ya Cecafa Challenge Cup, Waziri alikuwa mmoja kati ya nyota waliong’ara sana. Azam FC ikaamua kumpandia boti kwenda kumfuata. Ikumbukwe kuwa wachezaji wote hawa wawili pia walikuwa wakiwaniwa kwa udi na uvumba na vilabu vya Simba na Yanga na Azam FC ikawa na msuli wa kuweza kuwanasa.

Utasema nini kuhusu Khamis Mcha Viali nyota ambaye chama cha waandishi wa habari nchini TASWA walimjumuisha kwenye tuzo za Taswa akiwania kuwa mchezaji bora nchini. Tuzo ambayo ilichukuliwa na Shadrack Nsajigwa.

Ukifika Zanzibar na kuulizia jembe ambalo wazanzibari wanalihusudu hivi sasa kwenye eneo la kiungo basi utaambiwa Abdulghani Ghulam Ally, nyota ambaye baba yake ni mchezaji wa kimataifa wa zamani wa Zanzibar ambaye alipewa jina la Abdulghani kama zawadi kwa nyota mwingine wa Zanzibar ambaye ni kocha maarufu Abdulghani Msoma.

Ghulam anaaminika kuwa na kipaji cha hali ya juu na kama ilivyo kwa vyota wengine wa Zanzibar akina Nadir haroub, Abdi Kassim na Selemani kassim, ambao ilihitaji kuhamia ligi kuu ya bara kuweza kutambulika na kuingizwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania taifa Stars.

Usajili wa Azam FC haukuwa wa kutaka kushindana wala kukimbilia majina ila viwango kutokana na mahitaji ya timu na mapungufu yaliyojitokeza msimu uliopita na ulifanywa na kocha mwenyewe Stewart Hall bila kuingiliwa na mtu yoyote.

Katika nafasi ya Golikipa, Mwadini ally Mwadini na Obren Cuckovic watakuwa wakishindana kulinda nyavu za Azam FC zisiguswe. Kila mtu anajua ubora wa Obren na kipaji alichokuwa nacho kabla ya kuondoka nchini kadhalika Mwadini Ally ambaye Kocha Stewart Hall ana imani kubwa naye kutokana na kumfahamu na kufahamu uwezo wake.

 

Ibrahim Shikanda na Erasto Nyoni (upande wa kulia) na waziri Salum Omar na malika Philip Ndeule (upande wa kushoto) watatengeneza mbavu za chini za Azam FC huku Beki nyota wa King Faisal Babes ya Kumasi Ghana Nafiu Awudu akishirikiana na Aggrey Morris, Luckson Kakolaki na beki toka Kagera Sugar Said Morrad kutengeneza “The back four” ukuta wa Azam FC ambao unatarajia kupunguza idadi ya magoli ya kufungwa.

Ni matumaini ya kocha Sewart Hall kuwa kiwango cha makinda Himid Mkami na Salum Abubakar kitakuwa kimeongezeka kutokana na sasa kuwa na uzoefu wa kutosha ukichagizwa na mechi za kimataifa ambazo timu ya taifa U-23 inacheza hivi sasa chini ya Jamhuri kihwelu Julio.

Wachezaji hawa wataungana na Abdulhalim Humud, Jabir Aziz, Abdulghani Ghulam Abdallah na Ramadhan Chombo Redondo kutengeneza uti wa mgongo wa Azam FC msimu wa 2011/12.

Msimu uliopita Azam FC licha ya kushika nafasi ya tatu, ndiyo timu iliyofunga magoli mengi zaidi ikifunga magoli 41, Simba 40 na Yanga 32. Katika magoli hayo 41, magoli 36 yalifungwa na wachezaji watatu, Mrisho Ngasa 16, John Bocco 13 na Ramadhan Chombo Redondo 7. Azam FC imemuongeza Kipre Herman Tchetche ambaye ametwaa tuzo ya mfungaji bora wa Ivory Coast, Mchezaji Bora wa Ivory Coast na mchezaji bora wa ligi kuu ya Ivory Coast.

Mbali na Tchetche Azam FC pia imemuongeza Mshambuliaji wa nyota wa King Faisal Babes ambaye anashika nafasi ya tatu kwa kufunga magoli kwenye ligi kuu akiwa ameshafunga magoli 10 hadi hivi sasa Abdul Wahab. Wahab ambaye pia anachezea kikosi cha Ghana U-23, anaaminika kuwa mmoja kati ya washambuliaji bora kabisa wa kati nchini Ghana kwa sasa.

Hii namaanisha kuwa licha ya kuongoza kwa kufunga magoli msimu uliopita VPL, Azam FC imeongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji jambo linalomaanisha kuwa kikosi cha Azam FC kitakuwa bora zaidi ya msimu uliopita.

Idadi kamili ya wachezaji wa Azam FC 2011/12 ni kama inavyoonekana hapo chini.

 

Makipa

 • Mwadini Ally Mwadini
- Mafunzo Zanzibar
 • Obren Cuckovic
- Serbia
 • Daudi Mwasongwe


Walinzi wa Pembeni

 • Ibrahim Shikanda

 • Malika Ndeule

 • Waziri Omar
- Mafunzo Zanzibar
 • Erasto Nyoni

Walinzi wa Kati

 • Aggrey Ambross
 
 

 • Luckson kakolaki

 • Said Morrad – Kagera Sugar
 • Nafiu Awudu – Kingfaisal Babes Ghana

Viungo

 • Ibrahim Mwaipopo
 • Salum Abubakar 

 • Gulam Abdallah
- Malindi Zanzibar
 • Himid Mao Mkami

 • Ramadhani Chombo

 • Abdulhalim Humud 
- Simba SC
 • Jabir Aziz Stima (ana ruhusa ya klabu kwenda Norway)

Washambuliaji  wa pembeni

 • Mrisho Ngasa

 • Jamal Mnyate

 • Khamis Mcha 
- Zanzibar Ocean Vier
 • Suleimani Kassim
 • Kipre Herman Tchetche (J.C.A-T) Ivory Coast

 

Washambuliaji wa kati

 • John Bocco

 • Zahoro Pazzi
- African Lyon
 • Abdul Wahab Yahya – King Faisal Babes Ghana

 

Pia kwenye kikosi hicho wamo chipukizi wa Azam Academy ambao ni Daudi Mwaisongwe, Ibrahim Rajab Jeba, Omar Mtaki, na Wandwi Willium