Uongozi wa Azam FC umezionya timu zinazohitaji wachezaji wa timu hiyo kufata taratibu za uhamisho na si kuongea na wachezaji.

Akizungumza na waandishi wa habari klabuni leo asubuhi, Makamu mwenyekiti wa Azam FC, Said Mohamed amesema kuongea na mchezaji ni kosa kulingana na sheria za mpira wa miguu hasa kwa mchezaji aliye na mkataba na klabu.

Kauli hiyo imetolewa siku chache baada ya kupatikana kwa taarifa kuwa klabu ya Yanga inafanya mazungumzo na winga Mrisho Ngasa jambo ambalo ni kinyume na sheria na kanuni za mpira wa miguu.

“Ngasa ni mchezaji wetu, wanaomuhitaji wanatakiwa kuzungumza na klabu na sio mchezaji, kuzungumza na mchezaji ni kosa na kama tukichukua sheria wanashitakiwa, mazungumzo yote yanatakiwa kuzungumza na klabu.” alisema Mohamed.

Makamu aliongeza kuwa kutokana na taarifa hizo uongozi umemuweka chini mchezaji Ngassa na kumweleza taratibu zote zilizopo katika mkataba wake ikiwemo kutoruhusiwa kuzungumza na klabu yoyote.

Naye Ngassa alitoa kauli kuwa kuanzia sasa hatakubali kuongea na klabu yoyote hadi watakapofikia makubaliano na Azam FC, kulingana na mkataba wake unavyosema.

“Jana niliitwa na uongozi wa klabu, wakanielewesha baadhi ya taratibu zilizopo katika mkataba wangu, hivyo sitakiwi kuongea chochote na timu yoyote inayonihitaji inatakiwa kuongea kwanza na klabu ndio niende kuichezea.” Ngassa.

Ngassa aliongeza kuwa hana tatizo la kwenda klabu yoyote bali klabu inatakiwa kumalizana na Azam FC ili kuruhusiwa kuondoka, lakini kama hawatafanya hivyo atabaki kuwa mchezaji wa Azam FC.

Tangu kujiunga kwa Ngassa katika klabu ya Azam FC kwa mkataba wa miaka mitatu 2010-2013 akitokea klabu ya Yanga, klabu hiyo imekaririwa ikitoa tamko mara kwa mara la kumhitaji mchezaji huyo ikiwemo kuandika barua za kumuhitaji kwa mkopo.

Kumbukumbu za Azam FC zinaonyesha Nov 9 mwaka jana walipokea barua ya maombi kwa mchezaji huyo kucheza kwa mkopo lakini haikukubaliwa, na baadaye wakaandika barua ya kumtaka arejee katika timu hiyo kwa dau la shilingi mil 25 kiasi ambacho ni sawa na nusu ya gharama za kumununua mchezaji huyo.