Azam FC leo imekamilisha usajili wa mchezaji wa kimataifa wa Ivory Coast Kipre Herman Tcheche na kufanya idadi ya wachezaji wa kigeni kufikia watatu baada ya kumbakisha nahodha wake Ibrahim Shikanda na kumsajili golikipa wa zamani  wa Yanga Mserbia Obren Cockovic.

Kipre Tchetche, mfungaji bora wa mashindano ya CECAFA Tusker Challenge Cup yaliyofanyika jijini Dar es Salaam mwaka jana ambaye alikuwa akiingia kama mchezaji wa akiba kwenye  kikosi cha Ivory Coast na kuisaidia Ivory Coast kufika fainali baada ya kufunga magoli manne kati ya mechi tano alizoshuka dimbani.

Kipre Tchetche ambaye ni pacha wa mchezaji mwingine wa kimataifa wa Ivory Coast  Kipre Balou, alishinda tuzo za mchezaji bora wa ligi kuu ya Ivory Coast msimu uliopita baada ya kufunga magoli 14 kati ya mechi 20 alizoichezea timu yake ya Jeunesse Club d'Abidjan Treicheville (J.C.A-T) na kuisaidia klabu yake kushika nafasi ya pili kwenye ligi kuu.

Sasa azam FC imebakisha nafasi mbili ambazo ni beki wa kati na mshambuliaji wa kati ambapo inakamilisha usajili wa wachezaji hao kutoka nchini Ghana.