John Bocco na Mrisho Ngasa wameweka rekodi mpya ligi kuu ya bara baada ya kufunga magoli 10 katika mechi 11 za mzunguko wa pili. Hakuna goli la penati wala faulo toka kwa John Bocco mshambuliaji mrefu anayeaminika kuwa bora kuliko wote nchini kwa sasa.

Mrisho Ngasa ambaye ndiye mchezaji mwenye thamani kubwa nchini na ambaye analipwa pesa nyingi zaidi ya mchezaji yoyote nchini yeye kabeba tuzo ya ufungaji bora kwa kufunga magoli 16 huku Bocco akiwa na magoli 12, goli moja nyuma ya Gaudensi Mwaikimba wa Kagera Sugar.

Katika raundi ya kwanza ya ligi kuu Tanzania, wachezaji hawa walicheza kama washambuliaji pacha na Ngasa alifunga magoli sita huku Bocco akifunga magoli mawili tuu tena kwenye mechi ya ufunguzi wa ligi kuu mjini Arusha.

Kocha mpya wa Azam FC Stewar Hall alibadili mfumo wa uchezaji akiamini kuwa Ngasa anaweza kuwa na madhara zaidi akitokea wingi ya kulia huku Bocco akichezeshwa katikati peke yake. Mabadiliko haya yamesaidia sana kuwezesha wachezaji hawa kufunga magoli 10 kila mmoja na kama si kuruhusu magoli mengi kufungwa kwenye goli letu pengine leo tungekuwa na hadithi tofauti.

Azam FC imefunga magoli 41, magoli mengi kuliko timu yoyote ligi kuu licha ya watani wa jadi Simba na Yanga jana kununua karamu ya magoli ili waweze kutwaa ubingwa. Simba imefunga magoli 40 huku Yanga ikifunga magoli 32 pekee.

Lakini nyavu za Azam FC zimetikiswa mara 18 sawa na Kagera Sugar tofauti na Simba ambayo imefungwa mara 17 na Yanga mara saba tuu.

Azam FC imeshinda michezo 13, imetoka sare michezo minne na kufungwa mitano tuu lakini Yanga ambayo ni timu bingwa imeweka rekodi ya kipekee kwa kufungwa mchezo mmoja tuu na Mtibwa Sugar, ikitoka sare mara tisa na kushinda mara 12.

Katika mchezo wa jana mjini Morogoro. Azam FC ilishinda 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting magoli ya John Bocco kwa kichwa cha kuogelea aliyepokea pasi ya Mrisho Ngasa kabla na yeye kumlipa Ngasa kwa pasi safi na kumfanya Ngasa kufunga goli safi kwa mguu wa kulia.