Timu ya Azam FC inaelekea kumaliza msimu vizuri baada ya kuichapa Police Dodoma 3-1 katika mchezo wa ligi kuu uliochezwa leo uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

 

Azam FC imefanya mabadiliko kwa kumchezesha golikipa chipukizi Daudi Mwasongwe aliyeweza kuhimili mchezo huo, ilipata goli la kwanza dakika ya 22 kupitia kwa mshambuliaji John Bocco aliyeachia shuti la mbali na kutinga langoni mwa Police Dodoma.

 

Goli hilo lilidumu dakika 10 kabla ya mshambuliaji wa pembeni Mrisho Ngasa kuongeza goli la pili kwa mkwaju wa penati, baada ya mchezaji wa Police Dodoma,Frank Sindato kumfanyia madhambi.

 

Police Dodoma walianza kutafuta nafasi za kusawazisha magoli hayo kwa kufanya mashambulizi ya mara kwa mara lakini yaliokolewa vyema na golikipa chipukizi Daudi, matokeo hayo yalizipeleka timu zote mapumziko huku Azam FC ikiwa mbele kwa magoli mawili.

 

Kipindi cha pili Azam FC waliimarisha kikosi chake waliingia Kally Ongala na Jamal Mnyate waliochukua nafasi za Salum Aboubakar 'Sure Boy' na Ibrahim Shikanda, mabadiliko hayo yalileta nguvu mpya kwa Azam FC.

 

Dakika ya 53 Police Dodoma walipata goli la pekee kupitia kwa mchezaji Bantu Admin aliyepiga shuti lililotinga wavuni moja kwa moja.

 

Goli hilo lilidumu kwa dakika mbili, dakika ya 55 Mrisho Ngassa alikamilisha kalamu ya magoli kwa kuandika goli la tatu akiunga vyema pasi ya mchezaji John Bocco.

 

Azam FC imefikisha pointi 40 ikiwa katika nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi kuu unaongozwa na Simba yenye pointi 45 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 43.

 

Azam FC: Daudi Mwasongwe, Erasto Nyoni, Mutesa Mafisango/Malika Ndeule, Luckson Kakolaki, Aggrey Moris, Jabir Aziz, Ibrahim Shikanda/Jamal Mnyate, Salum Aboubakar/ Kali Ongala, John Bocco, Ramadhan Chombo na Mrisho Ngassa.