Kikosi cha Azam FC leo kimetoshana nguvu na timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 23 kwa kutoka sare ya 1-1, katika mchezo wa kirafiki uliochezwa katika uwanja wa Azam FC, Chamazi jijini Dar es Salaam .

 

Mchezo huo wa kwanza wa kirafiki kuchezwa katika uwanja wa Azam FC uliopo maeneo ya Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam ulihudhuriwa na mashabiki mbalimbali pamoja na viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini akiwepo kocha mkuu wa Taifa Stars, Jan B Poulsen.

 

U-23 wamecheza mchezo huo ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao kwa ajili ya kuanza kucheza mechi za kufudhu kucheza fainali za mashindano ya Olympic yanayotarajia kufanyika nchini Uingereza, timu hiyo itacheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Cameroun tarehe 27 mwezi March.

 

Katika mchezo wa leo U23 wamepata kipimo kizuri kwa kucheza na timu yenye uwezo ya Azam FC, walikuwa wa kwanza kupata goli katika dakika ya 28 ya mchezo huo kupitia kwa mchezaji Vantlaus John aliyemalizia kazi nzuri ya Abdul Gulam.

 

Azam FC walicheza wakiwa na lengo la kuipa mazoezi timu hiyo inayokabiliwa na mchezo mgumu, Azam walicheza kikosi kamili lakini hawakuweza kutikisa nyavu za timu hiyo, hivyo hadi mapumziko U23 walikuwa mbele kwa goli moja.

 

Kipindi cha pili mchezo ulikuwa mzuri na wa nguvu kwa timu zote, dakika ya 68 Ramadhan Chombo ‘Redondo’ alisawazisha goli hilo kwa kichwa kwa kucheza vizu pasi aliyopewa na mshambuliaji Peter Senyonjo aliyeingia kuchukua nafasi ya John Bocco.

 

Katika mchezo huo mchezaji Kally Ongala alipewa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu mchezaji wa U23 Amour Suleiman katika dakika ya 84.