Dakika 90 za mchezo kati ya Azam FC na Mtibwa Sugar umekamilika kwa timu hizo kutoka sare ya 2-2, katika mchezo wa ligi kuu uliochezwa leo uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam .

 

Magoli yote manne yalipatikana kipindi cha pili cha mchezo huo, huku kipindi cha kwanza kilishuhudia mchezo mkali kutoka kwa timu zote mbili zikitoshana nguvu kwa kucheza kandanda la kuzuia na kushambulia.

 

Kipindi cha pili kilikuwa cha kutafuta ushindi kwa timu zote, dakika ya 53 mshambuliaji John Bocco aliandika goli la kwanza kwa Azam FC na kufikisha idadi ya magoli 9 katika orodha ya wafungaji inayoongozwa na Mrisho Ngassa mwenye jumla ya magoli 13.

 

Baada ya goli hilo Mtibwa Sugar walibadilika na kuanza kucheza mchezo wa kasi kutafuta goli la kusawazisha wakafanya mabadiliko dakika ya 59 alitoka Vicent Barnabas akaingia Masoud Ally wakati Azam FC alitoka Seleman Kassim ‘Selembe’ nafasi yake kuchukuliwa na Jamal Mnyate.

 

Mabadiliko hayo kwa timu zote yaliongeza uhai na kuleta maafa ndani ya dakika nne kupatikana kwa magoli matatu, dakika ya 66, Mtibwa Sugar kupitia kwa mchezaji Thomas Morris alisawazisha goli hilo akiunga pasi ya Salum Machaku.

 

Dakika mbili baadaye (dk 68) mshambuliaji Mrisho Ngassa aliipatia Azam FC goli la pili, baada ya kumalizia kazi nzuri iliyofanywa na Jamal Mnyate aliyempatia mpira Ramadhani Chombo ‘Redondo’ aliyetoa pasi ya mwisho kwa Ngassa.

 

Dakika moja baadaye (dk 69), kiungo wa Mtibwa Sugar Shaaban Nditi alisawazisha goli hilo kwa kichwa na kumuacha golikipa wa Azam FC Jackson Chove akiwa haamini kilichotokea.

 

Azam FC ilishuka katika mchezo wa leo ikiwa na kumbukumbu ya kuifunga mtibwa Sugar 4-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza katika uwanja wake wa nyumbani wa Manungu, mjini Morogoro.

 

Matokeo hayo timu hizo zimegawana pointi mojamoja, Azam FC inabaki nafasi ya tatu ikiwa na pointi 37 wakati Mtibwa Sugar ikisimama nafasi ya nne ikiwa na pointi 31, huku Simba wakiongoza ligi kwa pointi 44 na kufuatiwa na Yanga yenye pinti 40.

 

Kocha mkuu wa Azam FC Stewart Hall amesema mchezo huo ulikuwa mgumu sana , kwani Mtibwa Sugar walicheza kwa kulinda goli muda wote.

 

“unapocheza na timu inayolinda goli muda mrefu inakuwia vigumu kupata ushindi hivyo kujikuta unacheza sana , nashukuru wachezaji wamepata nafasi na wameitumia vyema” Stewart.

 

Aidha kocha Stewart amesema matokeo ya mchezo huo yanampa matumaini ya kuweza kushika nafasi ya pili msimu huu wa ligi kuu, ikiwa atapata ushindi katika mechi zake zilizobaki huku Yanga ikipoteza hata mchezo mmoja.

 

Azam FC, Jackson Chove, Malika Ndeule, Mutesa Mafisango, Erasto Nyoni, Aggrey Moris, Jabir Aziz, Mrisho Ngassa, Salum Aboubakar, John Bocco, Ramadhan Chombo, Selembe/ Mnyate.

 

Mtibwa Sugar, Omary Ally, Juma Adul, Yusuh Nguya, Oadia Mungusa, Dickson Daud, Shaaban Nditi, Julius Mrope/Faustin Lukoo, Juma Mpakala/Monja Liseki, Husein Javu, Machaku na Vicent Barnabas/Masoud Ally.