Timu ya Azam FC inayopigana kufa na kupona pamoja na Simba na Yanga kuwania nafasi mbili za juu katika msimamo wa ligi kuu ili kuiwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa imeshaingia kambini na kesho itajitupa kwenye uwanja wa Uhuru kujaribu kupata pointi 3 muhimu toka kwa wakata miwa wa Turiani Manungu, Mtibwa Sugar.

Wakati Azam FC ikitinga kambini, kocha mkuu wa Azam FC ameiambia tovuti ya Azam FC kuwa anakabiliwa na majeruhi na kadi na atalazimika kukipangua kikosi chake. Ibrahim Mwaipopo atakosa mechi hii kutokana na kuwa na Kadi Nyekundu, Mutesa Mafisango na Ramadhani Chombo Redondo wana majeruhi ingawa wanaweza kuanza lakini nahodha Ibrahim Shikanda atakuwa jukwaani kutokana na kukabiliwa na majeruhi makubwa.

Azam FC iliyo na wachezaji nane (8) kwenye kikosi cha timu ya taifa ya vijana U-23 angalau imefanikiwa kuwapata wachezaji watatu ambao ni Himid Mao, Salum Abubakar na Jamal Mnyate lakini wachezaji hawa hawaoneshi kuwa fit 100% kutokana na kufanya mazoezi magumu na ya kukimbia kwenye kambi ya Timu ya Taifa.

Selemani Kassim Selembe yeye atakuwa akirejea uwanjani baada ya kukaa benchi kwa muda na Erasto Nyoni huenda akacheza upande wa kulia na kumpisha Luckson Kakolaki katikati acheze na Aggery Morris

Kambi ya Mazoezi ya Azam FC imekuwa yenye furaha sana na wachezaji wanaonesha ari ya kutaka kushinda mechi hii muhimu ambayo kama watashinda watakuwa wamevuka mtihani wa kwanza mgumu sana kwenye ratiba yake. Mtihani wa pili itakuwa klabu ya Yanga ambayo nayo kama Azam FC inawania nafasi ya kuwakilisha nchi.

Baada ya mazoezi ya leo asubuhi, kikosi kitakachoanza mechi ya keshi kitakuwa kama ifuatavyo

1. Jackson Chove

2. Malika Philip Ndeule

3. Mutesa Patrick Mafisango

4. Aggrey Morris

5. Erasto Nyoni

6. Jabir Aziz

7. Mrisho Ngasa

8. Salum Abubakar

9. John Bocco

10. Ramadhan Chombo

11. Selemani Kassim