Mrisho Ngassa wa Azam FC anazidi kuongoza wafungaji katika mechi ya ligi kuu baada ya  kufikisha idadi ya magoli 12, katika mchezo wa leo dhidi ya Majimaji FC ambao ulikamilika kwa sare ya 1-1, mchezo uliochezwa uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam .

Mchezo huo ulizikutanisha timu hizo huku Majimaji FC wakicheza mchezo ambao haukutegemewa na watu wengi na kufanya mashabiki kujiuliza tatizo liloikabili timu na kuwa ya pili kutoka chini.

Azam FC kama kawaida yao walicheza mchezo mzuri unaoeleweka kwa kutoa pasi zilizokuwa na maana, walipata goli dakika ya 19 ya mchezo huo kupitia kwa mkwaju wa penati uliopigwa na Mrisho Ngassa baada ya golikipa wa Majimaji FC Said Mohamed kumuangusha kiungo wa Azam FC, Ramadhani Chombo katika eneo la hatari.

Kipindi chote cha kwanza Azam FC walitoa mashambulizi mara kwa mara lakini hayakuweza kuongeza goli jingine kwani wachezaji Ngassa na Chombo na John Bocco walipoteza nafasi kwa kupiga nje au kuokolewa na kipa wa Majimaji FC.

Kipindi cha pili kilikuwa cha kasi kwa timu zote, Majimaji FC waliweza kutumia vyema dakika za mwanzo za kipindi cha pili na kuweza kusawazisha goli hilo kwa kichwa kilichopigwa na mchezaji mkongwe wa timu hiyo Everist Maganga.

Baada ya goli hilo mpira ulibadilika na kuwa wa kasi zaidi Azam FC waliendelea kushambulia lakini haikuwa bahati kwao, walifanya mabadiliko alitoka John Bocco akaingia Peter Ssenyonjo na kutoka Jamal Mnyate na nafasi yake kuchukuliwa na Himid Mao ambao walibadili mchezo lakini wakashindwa kubadili matokeo.

Majimaji nao hawakuwa nyuma kuimarisha kikosi chao baada ya kusawazisha goli hilo walianza kulinda goli lao wakiombea kupata japo hiyo pointi moja walifanya mabadiliko walitoka Issa Ismail, Paul Mgemwa na Patrick Betwel na nafasi zao kuchukuliwa na Peter Mapunda, Shabir Issa na Gabriel Zacharia.

Matokeo ya mchezo huo Azam FC inabaki nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi kuu kwa kuwa na pointi 36 nyuma ya Simba yenye pointi 37 huku Yanga ikiongoza kwa pointi 38, Majimaji imeongeza pointi moja na kuwa nafasi ileile ya pili kutoka chini kwa kufikisha pointi 12.

Baada ya mchezo huo kocha wa Azam FC, Stewart Hall amesema hakufurahishwa na matokeo ya mchezo huo, lakini wachezaji wamecheza kwa uwezo wao kwani Majimaji haikuwa timu rahisi kama watu wanavyodhani.

“Kwa kweli sijafurahishwa na matokeo hayo, hatukutakiwa kutoka sare ya aina yoyote ile, timu imepata nafasi nyingi sana za kufungwa hasa kipibdi cha kwanza lakini haikuzitumia vizuri.” Stewart.

Kikosi Azam FC:Jackson Chove, Ibrahim Shikanda, Mutesa Mafisango, Erasto Nyoni, Aggrey Moris, Jabir Aziz, Mrisho Ngassa, Salum Aboubakar, John Bocco/ Peter Ssenyonjo, Ramadhani Chombo na Jamal Mnyate/Himid Mao.

Majimaji FC:Said Mohamed, Mohamed Kijuso, Paul Ngalema/Shabir Issa, Evarist Maganga, Patrick Betwel/Gabriel Zacharia, Isa Ismail/Peter Mapunda, Juma Mpola, Mohamed Mpopo, Ulimboka Mwakingwe, Kasim Kilungo na Lulanga Mapunda.