Imani kuwa Simba na Yanga ndizo timu kubwa pekee nchini inazidi kufa kutokana na matukio ya hivi karibuni ambayo yamekuwa yakitokea upande wa Azam FC.

Tayari Azam FC imeshaanza kupokea lundo la mashabiki waliokuwa wa Simba na Yanga ambao wamechoka na migogoro isiyoisha na maendeleo duni  vilabuni mwao, mashabiki hao wamekuwa wakinunua jezi za Azam FC kwa kasi kubwa

Wiki iliyopita Azam FC iliweka historia nyingine kwa kuongoza ligi zikiwa zimesalia mechi sita ligi kuisha, Azam FC haijawahi kuongoza ligi katika historia yake lakini cha kuvutia zaidi ni kwamba Tangia Mtibwa Sugar ilivyowahi kufanya hivyo miaka 10 iliyopita, hakuna timu nyingine iliyowahi kufanikiwa kufanya hivyo nje ya Simba na Yanga

Kama hayo hayatoshi, wiki iliyopita watangazani wa DSTV Supersports walimhoji kocha mkuu wa Azam FC ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Match Highlights na vipindi vyao. Azam FC, Simba na Yanga zinakuwa timu pekee zilizohojiwa na kituo hiki cha televisheni na hii ina maana kuwa DSTV – Supersports wanaipa hadhi ya kutosha Azam FC

Watangazaji wa kituo hicho tayari wameshaomba nafasi nyingine ya kutembelea center ya mazoezi ya Azam FC siku za usoni ili kutengeneza kipindi maalum na sidhani kama wameshaomba kufanya hivyo au kutembelea Center za Simba na Yanga.

Hili la Mechi mbili tuu za ligi kuu kurushwa live on DSTV- Supersports na mechi hizo kuhusisha Azam FC, Simba na Yanga pia linaonesha kuwa Azam FC inahadhi kubwa machoni pa mangwiji hawa wa kurusha matangazo ya mpira barani Afrika ambao pia walirusha live kombe la dunia lililopita.

Kuna jambo lingine muhimu ambalo inabidi nilitaje, kwenye mashindano ya CECAFA Challenge Cup miaka miwili iliyopita, Azam FC ndiyo klabu iliyokuwa na wachezaji wengi zaidi kwenye timu za Burundi, Kenya, Uganda, Zanzibar, na Tanzania Bara.

Katika mechi ya leo Azam FC itakuwa ikijaribu kurejea tena kileleni mwa ligi hiyo ambapo endapo itashinda itafikisha pointi 38 na kuongoza ligi. Pointi 38 ni idadi ya juu kabisa ya pointi kuwahi kufikiwa na Azam FC tangia ianzishwe miaka minne iliyopita.

Pia ikumbukwe kuwa Azam FC itakuwa ikijaribu kupata ushindi wa sita mfululizo na hii ni rekodi nyingine kwa klabu hii lakini pia katika raundi hii ya pili ya ligi kuu, hakuna klabu iliyofanikiwa kushinda mechi japo tano mfululizo zaidi ya Azam FC.

Katika mechi ya leo, Azam FC itateremsha kikosi chake kilichoiua Simba isipokuwa Ibrahim Mwaipopo ambaye ana kadi nyekundu na nafasi yake itachezwa na Jabir Aziz.

Azam FC itapangwa kama ifuatavyo

 1. Vladmir Niyonkuru
 2. Ibrahim Shikanda
 3. Mutesa Mafisango
 4. Aggrey Morris
 5. Erasto Nyoni
 6. Jabir Aziz
 7. Mrisho Ngasa
 8. Salum Abubakar
 9. John Bocco
 10. Ramadhan Chombo
 11. Jamal Mnyate