Kadri muda unavyozidi kuongezeka kikosi cha Azam FC kinazidi kujiimarisha, baada ya kufanikiwa kuifunga timu ya Villa Squad 3-2 katika mchezo wa kirafiki uliochezwa leo asubuhi, uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

 

Azam FC imeshinda mchezo huo ikitumia wachezaji wengi wa kikosi cha pili na kuipa mazoezi timu hiyo iliyopanda tena kucheza ligi kuu msimu ujao wa 2011/2012 baada ya kushuka daraja misimu miwili iliyopita.

 

Wachezaji wa Azam FC wasiocheza mechi hiyo ni wale wa kikosi cha kwanza ambao ni golikipa namba moja, Vladimir Niyonkuru, nahodha Ibrahim Shikanda, washambuliaji John Bocco na Mrisho 'Uncle' Ngassa, walinzi Erasto Nyoni na Aggrey Moris na viungo Jabir Aziz na Ramadhan Chombo 'Redondo'.

 

Kikosi cha mchezo wa leo kilipata goli la kwanza dakika ya pili ya mchezo lililofungwa na mshambuliaji wa kimataifa kutoka Uganda, Peter Ssenyonjo aliyeachia chuti la umbali mrefu lililotinga nyavuni mwa Villa Squad.

 

Villa Squad waliweza kusawazisha goli hilo ya 14 ya mchezo huo kupitia kwa mchezaji Rashid Roshwa aliyetumia vyema uzembe wa mabeki wa Azam FC.

 

Dakika 16 baadaye mchezaji wa Azam FC Seleman Kassim 'Selembe' aliifungia timu yake goli la pili kwa kuunga vyema mpira uliopigwa na Ssenyojo katika dakika ya 30 ya mchezo huo.

 

Ssenjonjo akiwa amerejea uwanjani siku chache baada ya kusumbuliwa na malaria, aliandika goli la tatu kwa Azam FC akipigwa kichwa mpira uliochongwa na mshambuliaji mwenye kasi ya nguvu Jamal Mnyate.

 

Mchezaji Mutesa Mafisango ameendelea kufanya vizuri katika nafasi ya ulinzi akishirikiana na viungo Ibrahim Mwaipopo na Salum Aboubakar, pia wachezaji Chipukizi Sino Agustino, Ibrahim Jeba, Ally Mkuba, Himid Mao, Fred Cosmas na LUckson Kakolaki wameonyesha uwezo wao.

 

Villa Squad wakiwa hawaamini kama kikosi chao ndicho kilifanyikiwa kuingia ligi kuu kwa kufungwa na Azam FC iliyojaa wachezaji chipukizi, walipata goli la pili dakika ya 65 ya mchezo huo kupitia kwa mchezaji Shaaban Juma.

 

Kikosi Azam FC: Jackson Chove/Wandu Willium, Ibrahim Mwaipopo/Himid Mao, Salum Aboubakar/Ally Mkuba Sisoko, Sino Agustino/Cosmas Lewis, Mutesa Mafisango/Ibrahim Jeba, Luckson Kakolaki, Peter Senyonjo/Sino, Malika Ndeule na Tumba Swed.