Baada ya kusumbuliwa na tatizo la goti kwa muda mrefu mchezaji wa Azam FC Samir Haji Nuhu anatarajia kwenda nchini India kupata matibabu zaidi.

Akithibitisha safari hiyo ya matibabu kwa mchezaji huyo, kocha mkuu wa Azam FC, Stewart Hall amesema daktari ameruhusu akafanyiwe upasuaji nchini humo na anatarajiwa kuondoka wiki ijayo.

“Tatizo ni kubwa, kitaalamu linaitwa 'Interior Cruciate Ligament -ACL' akipatiwa tiba nchini India atarudi katika hali yake ya kawaida, kwa sasa daktari anafatilia utaratibu wa Visa ya kwenda nchini humo.” amesema Stewart.

Ameongeza kuwa wachezaji wengine waliokuwa majeruhi wameanza mazoezi mepesi huku wale wengine wakiwa katika mazoezi makali kwa maandalizi ya mechi zijazo.

Kocha amewataja wachezaji waliokuwa majeruhi na kukosa mechi zaidi ya mbili ni Mutesa Mafisango, Erasto Nyoni na golikipa namba moja wa timu hiyo Vladimir Niyonkuru.

Akiizungumzia mechi ijayo dhidi ya timu ya Majimaji amesema ni timu nzuri yenye ushindani, wanajiandaa zaidi kuweza kukabiliana nayo kwani wanaheshimu kila timu wanayocheza nayo.

“inaonekana timu ngumu japo sijacheza nayo, nimeangalia matokeo yake na mwenendo wake inaonekana timu yenye upinzani mkubwa, nawaandaa zaidi wachezaji wangu waweze kufanya vizuri katika mchezo huo, hatuidharau hata kama iko chini katika ligi.” Stewart.