Uwezo na jitihada zinazoonyeshwa na wachezaji wa Azam FC zimeipelekea timu hiyo kuongoza ligi kuu ya Vodacom baada ya kushinda mechi ya tano mfululizo kwa kuifunga JKT Ruvu 2-0 katika mchezo ulichezwa leo jioni uwanja wa Uhuru, jijini, Dar es Salaam .

 

Azam FC imeitoa Yanga na kuongoza msimamo wa ligi hiyo kwa kuwa na pointi 35 sawa na Yanga wakizidiana idadi ya tofauti ya magoli, Azam FC imefikisha magoli 21 kwa kufunga 32 na kufungwa 11  huku Yanga wakiwa na tofauti ya magoli 18 kwa kufunga 22 na kufungwa manne tu, nafasi ya tatu inashikiliwa na bingwa mtetezi Simba SC.

 

Timu hiyo mpya katika ligi kuu imeweza kufunga mechi tano mfulilizo baada ya kuzifunga timu za Simba 3-2, African Lyon na Toto African 3-0 kila moja na AFC 5-1, Azam FC imepoteza mchezo mmoja ikifungwa 2-1 na timu ya Kagera Sugar.

 

Azam FC imeonekana kuutumia vyema uwanja wa Uhuru ilipata goli la kwanza dakika ya 42 kupitia kwa kiungo wa kati, Ibrahim Mwaipopo aliyeachia shuti la umbali mrefu na kumuacha golikipa namba moja wa JKT Ruvu, Shaaban Dihile ikiwa haamini kilichotokea.

 

Goli hili lilidumu hadi mapumziko, mchezo wa kipindi cha kwanza ulikuwa mgumu kwa timu zote kwani zilionekana kucheza mchezo unaofanana hivyo kushambuliana mara kwa mara.

 

Kipindi cha pili kilipoanza timu zote zilifanya mabadiliko kwa nyakati tofauti walianza JKT Ruvu kuwatoa Haruna John, Bakari Kondo na Sostenes Manyasi na nafasi zao kuchukuliwa na Akilimali Yahya, Pius Kasambale na Amos Mgisa ambao walibadili mchezo na kuongeza nguvu kwa tmu hiyo.

 

Azam FC waliwapeleka benchi John Bocco, Himid Mao na Ramadhan Chombo ‘Redondo’ huku wachezaji Peter Ssenyonjo, Jamal Mnyate na Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ wakichukua nafasi zao na kufanya vizuri, kuziba nafasi ya mchezaji Ibrahim Mwaipopo aliyetolewa kwa kadi nyekundu.

 

Mwamuzi wa mchezo huo Oden Mbaga alimtoa Mwaipopo baada ya kumfanyia madhambi mchezaji wa JKT Ruvu Bakari Kondo katika dakika ya 59 ya mchezo huo, vile vile wachezaji Luckson Kakolaki na Himid Mao walipewa kadi za njano.

 

Goli la pili la Azam FC lilipatikana katika dakika ya 73 baada ya mchezaji wa JKT Ruvu Shaibu Nayopa kujifunga mwenyewe, Nayopa aliunganisha mpira wa kona uliopigwa na nahodha wa Azam FC Ibrahim Shikanda.

 

Kocha mkuu wa Azam FC Stewart Hall ameridhishwa kiwango cha wachezaji wake kwa vipindi vyote na kukubali uwezo JKT Ruvu walioonyeha katika mchezo huo na kusema ni mchezo bora kwake.

 

“Tangu nianze kuifundisha Azam FC na kucheza mechi sita, mechi ya leo ni mechi nzuri na bora kwangu, timu yangu haijawahi kukutana na timu yenye uwezo kama JKT Ruvu, wamecheza mchezo mzuri sana nawapongeza wachezaji wangu”amesema Stewart.

 

Stewart ameongeza kuwa japokuwa timu inakabiliwa na majeruhi wengi kutolewa kwa mchezaji Mwaipopo kulibadili mfumo mzima wa timu, wachezaji wakawajibika ipasavyo kwa kucheza kwa moyo mmoja na kupata nafasi nyingi kitu ambacho sikukitegemea.

 

Azam FC: Jackson Chove, Ibrahim Shikanda, Malika Ndeule, Aggrey Moris, Luckson Kakolaki, Ibrahim Mwaipopo, Mrisho Ngassa, Jabir Aziz, John Bocco/Peter Ssenyonjo, Ramadhan Chombo/Jamal Mnyate na Himid Mao/ Salum Aboubakar ‘Sure Boy’.