Japokuwa Azam FC inakabiliwa na majeruhi wanne katika kikosi chake, wanatarajia kuendeleza ushindi katika mchezo wake wa kesho (Jumapili) dhidi ya timu ya JKT Ruvu kutoka mkoani Pwani, mchezo utakaochezwa uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salama.

 

Akizungumzia hali ya kikosi hicho, kocha mkuu wa Azam FC, Stewart Hall amesema majeruhi wamebadilisha mfumo wa timu hivyo wachezaji wengine watachukua nafasi zao kama ilivyo kuwa katika mechi iliyopita.

 

“Majeruhi wanaendelea kupata matibabu, tumefanya mazoezi na wachezaji wengine wamefanya vizuri, mchezo na JKT Ruvu tunauchukulia kama mgumu kwetu lakini tunatakiwa kushinda ili kuongeza pointi zaidi” Stewart.

 

Kocha huyo kutoka nchini Uingereza ameongeza kuwa timu imepata nguvu mpya baada ya mshambuliaji wa kimataifa kutoka nchini Uganda , Peter Ssenyonjo kurejea katika kikosi hicho baada ya kuwa nje ya uwanja kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa malaria.

 

Amesema wachezaji kama golikipa Jackson Chove, Himid Mao na Malika Ndeule walionyesha kiwango cha juu katika mchezo uliyopita hivyo timu bado iko imara na itaendelea kufanya vizuri.

 

Amewataja majeruhi kuwa ni golikipa namba moja wa kikosi hicho,Vladimir Niyonkuru, Erasto Nyoni, Samir Haji na Mutesa Mafisango.

 

Azam FC imefikisha pointi 32, imeshinda mechi nne mfulizo kwa kuwafunga Toto African  na African Lyon 3-0 kila moja, wakaifunga Simba 3-2 na kuwatesa AFC 5-1, Azam FC imepoteza mchezo mmoja tu katika mzunguko kwa kufungwa 2-1 na Kagera Sugar.