Timu ya Azam FC imeendeleza wimbi la ushindi baada ya leo kuifunga African Lyon 3-0 na kukaa katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu Tanzania bara ‘VPL’ kwa kuwa na pointi 32. Angalia hapa http://www.azamfc.co.tz/league_standings

 

Azam FC imepata ushindi huo katika mchezo namba 94 wa ligi kuu uliochezwa uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam .

 

Goli la kwanza la Azam FC limepatikana dakika ya 9 kupitia kwa mshambuliaji Mrisho Ngassa ‘Uncle’ aliyechonga mpira wa adhabu uliotikisa nyavu za African Lyon, baada ya wachezaji wa Lyon kumtendea madhambi mchezaji Ramadhani Chombo ‘Redondo’ wa Azam.

 

African Lyon ilionekana kuongeza juhudi za kutaka kusawazisha goli hilo lakini walizidiwa mchezo na Azam FC ambayo mabeki wa timu hiyo walikuwa imara kuweza kuwadhibiti vyema.

 

Azam FC ilifanya mabadiliko ya kwanza dakika ya 25 baada ya mlinzi mahiri Erasto Nyoni kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Luckson Kakolaki.

 

Mabadiliko katika kikosi cha Azam FC wachezaji Malika Ndeule na Himid Mao waliocheza kikosi cha kwanza, wameweza kumudu nafasi hizo vizuri kwani dakika ya 37, Himid Mao aliandika goli la pili kwa Azam FC  kufuatia shambulizi la ‘counter attack’ baada ya kupokea mpira wa mbali kutoka kwa Mrisho Ngassa aliyewakimbiza walinzi wa A. Lyon.

 

Matokeo hayo yaliipeleka Azam FC mapumziko ikiwa mbele kwa magoli 2-0 dhidi ya African Lyon.

 

Kipindi cha pili African Lyon ilifanya mabadiliko kwa kutoka Shaaban Aboma, Adam Kingwande na Mohamed Samata nafasi zao kuchukuliwa na Idrissa Rashid, Haji Dudu na Benedictor Jacob lakini mabadiliko hayo hayakuweza kuipa ushindi timu hiyo yenye maskani yake jijini Dar es Salaam .

 

Mabadiliko upande wa Azam FC walitoka Ibrahim Mwaipopo dk 62 na Himid Mao Mkami dk 72 nafasi zao kuchukuliwa vyema na Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ na Jamal Mnyate ambao walibadilisha mchezo na kuwa wa kasi zaidi.

 

Dakika ya 87 mchezaji mwenye uwezo wa pekee Ramadhan Chombo ‘Redondo’ alifunga idadi ya magoli kwa kuandika goli la tatu baada ya kuachia shuti lililotinga moja kwa majo wavuni akiunganisha pasi kutoka kwa Ngassa.

 

Mrisho Ngassa wa Azam FC amecheza katika kiwango cha juu kwa kutoa pasi za mwisho katika magoli mawili na kufunga goli la kwanza, upande mwingine wachezaji Jabir Aziz, Malika Mdeule, Himid Mao, Lackson Kakolaki na golikipa Jackson Chove wamemtendea haki mwalimu aliye waamini baada ya kufanya kazi nzuri sana leo.

 

Baada ya mchezo huo, Mrisho Ngasa anaongoza wafungaji kwa kufikisha jumla ya magoli 11 huku Ramadhani Chombo akifikisha goli la sita.

 

Kocha wa Azam FC Stewart Hall amezungumzia mchezo huo kwa kusema tmu yake haijacheza katika kiwango cha juu lakini amefurahi kwa kupata ushindi huo wa 3-0.

 

“Sijaona zile pasi nyingi kama za mwanzo nadhani hiyo imetokana na kuchezesha wachezaji wapya katika kikosi cha kwanza baada ya wengine kusumbuliwa na majeraha na malaria.” Alisema Stewart.

 

Stewart aliongeza kuwa amewasifu walinzi wa kikosi hicho kwa jithada za kuizuia African Lyon huku akisema viungo wamebadilika na kucheza katika kiwango kinachotakiwa.

 

Amewataja wachezaji Haji Nuhu na golikipa Vladimir Niyonkuru kuwa ni majeruhi wakati Peter Senyonjo na Mutesa Mafisango wakisumbuliwa na Malaria.

 

Azam FC iliyoshinda leo: Jackson Chove, Ibrahim Shikanda, Malika Ndeule, Nyoni/Kakolaki, Aggrey Moris, Mwaipopo/Sure Boy, Ngassa, Jabir Aziz, Chombo, John Bocco na Himid Mao/Jamal Mnyate.

 

Lyon: Noel Lucas, Aziz Sibo, Hamis Shengo, Zuber Ubwa, Bakari Nzige, Shaaban Aboma, Hamis Yusuph, Mohamed Samata, Adam Kingwande, Samwel Ngasa na Sunday Juma.