Mechi ya keshokutwa jumatano dhidi ya African Lyon itashuhudia mabadiliko matatu mawili yakiwa mapya kabisaa ambapo wachezaji Himid Mao na Malika Ndeule watakuwa wanufaikaji wakuu wa mabadiliko hayo.

Mabadiliko haya yatakuwa katika beki ya kushoto ambako Mutesa Patrick Mafisango amekuwa akiishilia nafasi hiyo kwa muda mrefu  lakini katika mechi ya Jumatano Kocha Stewart amesema atampanga Malika Philip Ndeule na mbele yake yaani wingi ya kushoto atampanga Himid Mao.

Badiliko lingine ambalo si jipya sana litamhusu Jabir Aziz, mchezaji aliyekuwa nyota wa mchezo kati ya Taifa Stars na Palestine na keshokutwa ataanza kwenye dimba la kati kutokana na Salum Abubakar kukosa mazoezi ya mwisho kutokana na mkewe kujifungua.

Akizungumza na Tovuti ya Azam FC baada ya mazoezi, kocha Sewart alisema, mchezaji Luckson Kakolali amebadilika sana na sasa yupo tayari kucheza lakini mwenzake Tumba Swedi  anapaswa kuongeza bidii.

Stewart alishangazwa na bidii aliyonayo Sino Agustino na akasema kunamabadiliko makubwa kiakili na kimchezo kwa Sino. Sasa anaonekana yupo tayari na anataka kucheza, hivi ndivyo ninavyotaka kuona toka kwa wachezaji wangu.

Stewat aliongeza kuwa wachezaji nyota kwake ni Jamal Mnyate na Himid Mao. Anasema Himid yupo katika dunia nyingine kabisa, ni mchezaji ambaye anajua kwa nini yupo Azam FC na anataka kwenda wapi, inatia moyo unapokuwa na wachezaji chipukizi wa aina ya Himid kwani unaweza kuwatumia kwenye mechi na kuwajengea uwezo zaidi bila kuathiri matokeo.

Kuhusu Jamal Mnyate, Stewart anasema, yule kijana ni wa ajabu sana, ana nguvu nyingi sana, akikaa mbele yako unahitaji greda kumtoa na miguu yake ina nguvu sana za kupiga mashuti. Kasi yake ni kama upepo. Uncle (Ngasa) anafanana sana na Jamal na huwa sina shaka kama Uncle anakuwa hayupo kwani Jamal Yupo na anaweza kuifanya kazi ya Uncle barabara.

Akizungumzia kikosi chake kwa ujumla anasema ukiondoa wachezaji wawili au watatu ambao bado anawaangalia mieneno yao. Wachezaji alionao anasema wana nidhamu sana na wana nia ya kutaka kushinda na hili ni muhimu sana kwenye timu. Kuna wachezaji wachache wanataka kuniharibia timu (anawataja) nimewaweka kwenye diary yangu nawapa muda na nawachunguza. Nitakapoamua kuwatimua ntawatimua kwani mwakani nataka kujenga kikosi bora chenye nidhamu.

Timu inaingia kambini leo kujiandaa na African Lyon na wachezaji Salum Abubakar pamoja na Mutesa Patrick Mafisango hawataingia kambini na wenzao kutokana na sababu mbalimbali yakiwemo matatizo ya kifamilia.