MABAO mawili ya kichwa ya kipindi cha kwanza ya mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, John Bocco na moja la mchezaji ghali zaidi nchini, Mrisho Ngassa yalitosha kuipa pointi tatu muhimu timu ya Azam na kuisogelea Yanga iliyo kileleni kwa tofauti ya pointi mbili baada ya kuichapa Toto African 3-0 katika pambano lililofanyika uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.

Wakati mashabiki wa soka nchini wakiwa na kumbukumbu ya tukio la wachezaji wa Azam kupiga pasi 39 bila ya wachezaji wa Simba kugusa katika pambano lililofanyika wiki mbili zilizopita, Azam waliwakosha tena mashabiki waliohudhria pambano lao dhidi ya Toto baada ya kufunga bao katika dakika ya kwanza ya mchezo wakipiga pasi zaidi ya 10 bila ya mpira kuguswa na Bocco kufunga kwa kichwa kwa umaridadi wa aina yake.

Bocco mwenye urefu wa futi 6.1 alimalizia kwa ustadi krosi iliyopigwa na mlinzi wa Kimataifa wa Kenya, Ibrahim Shikanda aliyepokea pasi ya tisa kutoka kwa wenzake huku wachezaji wa Toto wakiwa hawajagusa mpira huo tangu uanze.

Azam FC ambayo imehamia kwenye kiwanja chake cha mazoezi Chamanzi, baada ya hapo iliutawala mpira huku wachezaja Ibrahim Mwaipopo, Ibrahim Shikanda na Ramadhan Chombo waking’ara na kutoa burudani safi kwa mashabiki.

Katika mchezo wa leo Jabir Aziz alicheza kiungo cha katikati mbele na alicheza vizuri sana kama ilivyo kwa John Raphael Bocco ambaye alimfurahisha kila aliyefika uwanjani.

Uchezaji wa mabeki wa kati wa Azam FC Aggrey Chacha Morris na Erasto Nyoni bado uliendelea kuwa wa hali ya juu na uelewano wa uhakika.

Katikati ya kipindi cha kwanza, krosi safi tena ya Ibrahim Shikanda iliunganishwa vema kwa kichwa na John Bocco na kufunga goli lake la pili katika mechi ya leo likiwa goli lake la sita katika mechi tatu mfululizo akifunga magoli mawili kila mechi na hivyo kufikisha idadi ya magoli nane na sasa kuingia rasmi kwenye kinyang’anyiro cha kusaka kiatu cha dhahabu.

Hadi timu zinakwenda mapumziko Azam FC ilikuwa mbele kwa magoli mawili kwa bila

Kipindi cha pili, azam FC ilianza kupiga pasi zake za uhakika na kuutawala mchezo kwa muda mrefu.

Lakini ilapata balaa baada ya John Bocco kuugua tumbo ghafla na hivyo kutoka na nafasi yake kuchukuliwa na Mganda Peter Ssenyonjo

Kama hiyo haitoshi, beki wa kushoto wa Azam FC Mutesa Patrick Mafisango naye aliumia goti na nafasi yake ikachukuliwa na Maulid Boffu Ally.

Ilikuwa kama siku ya Ibrahim Shikanda kwani krosi yake aliyoipiga kunako dakika ya  80 ilitua kwenye mguu wa Mrisho Ngasa na kufunga goli la tatu na la mwisho kwa leo.

Ngasa kwa kufunga goli la tatu alifikisha goli la kumi na hivyo kufikisha magoli kumi na kuongoza kundi linalowania ufungaji bora akikaribiwa kwa karibu na Gaudensi Mwaikimba mwenye magoli tisa na John Bocco mwenye magoli nane

Azam FC iliwakilishwa na Vladmir Niyonkuru, Ibrahim Shikanda, Mutesa Patrick Mafisango/Mau Boffu, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Ibrahim Mwaipopo, Mrisho Ngasa, Jabir Aziz, John Bocco/Peter Ssenyonjo, Ramadhan Chombo, Selemani Kassim/Malika Philip Mdeule